Jafo ataka mikakati kulinda bonde Mto Nile

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akifungua Mkutano ya Mabaraza ya Mawaziri wa Maji wa Nchi za Bonde la Mto Nile jijini Dar es Salaam leo Agosti 19, 2022.

NCHI za Ushirikiano wa Mpito wa Bonde la Mto Nile (NBI) zimetakiwa kutengeneza mikakati ya kulinda rasilimali maji ya Bonde la Mto Nile ili kulinda chanzo hicho cha maji kinachotumiwa na watu zaidi ya milioni 278 wanaoishi katika bonde hilo.

Kauli hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Sulemani Jafo (pichani) wakati akifungua mkutano wa 30 wa Baraza la Mawaziri wa Nchi za Ushirikiano wa Bonde la Mto Nile uliofanyika jijini hapo.

Jafo aliyemwakilisha Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alisema nchi za NBI ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Misri na Sudan zinapaswa kuendelea kushirikiana katika kulinda chanzo cha maji ya mto huo ambacho ni muhimu kwa uchumi wa mataifa hayo.

Advertisement

Alisema changamoto ya sasa inayokabili nchi za ushirikiano wa mto huo ni mabadiliko ya tabianchi ambayo yameleta maafa katika nchi zinazotumia maji ya mto huo.

Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Anthony Sanga alisema Tanzania imepewa heshima ya kuandaa mikutano hiyo ya Mabaraza ya Mawaziri wa Maji wa Bonde la Mto Nile iliyoanza Agosti 18 na kumalizika jana lengo likiwa ni kuendeleza ushirikiano wa nchi wanachama.

Mkutano huo ulitanguliwa na Baraza la Mawaziri wa Maji wa nchi za Mashariki (ENSAP) unaofanyika Agosti 18, ukifuatiwa na Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa Bonde la Mto Nile (Nilecom) pamoja na mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Maji Ukanda wa Maziwa Makuu (Nelcom) uliofanywa na kuhitimishwa jana.

Katika mikutano hiyo Tanzania pamoja na kuwa mwenyeji wa mkutano huo imepokea kijiti cha uenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa Bonde la mto huo kwa mwaka 2022/2023 kutoka Sudan Kusini.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBI, Sylvester Temu alisema ushirikiano huo umekuwa na manufaa makubwa kwa nchi zote 10 zinazounda Bonde la Mto Nile.

Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi, Dk Rurema Deo-Guide alisema Burundi itaendelea kushirikiana na nchi za NBI kuhakikisha manufaa ya Mto Nile yanakuwa kwa wote. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alizitaka nchi washirika wa bonde hilo kuhakikisha zinaendeleza umoja na ushirikiano kuimarisha rasilimali ya maji katika ukanda huo na kuzilinda kwa sababu maji hayana mbadala.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *