Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo amesema katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, Wananchi wanapaswa kutunza miradi inayotekelezwa na Serikali.
Waziri Jafo ametoa wito huo wakati akizindua miradi ya visima vya maji, vitalu nyumba, josho la kuogeshea mifugo na mashine ya kukamua mafuta ya alizeti wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma hivi karibuni, miradi inayotekelezwa kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR).
Akizungumza na wananchi wakati wa ziara hiyo, Dk Jafo amesema Ofisi ya Makamu wa Rais imeamua kutenga fedha ili kutekeleza mradi hiyo kwa maeneo mbalimbali yenye ukame ikiwemo Mpwapwa ili kutatua changamoto zinazotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Ndugu zangu mradi huu una thamani kubwa tumeona wenyewe hapa kupeleka maji zaidi ya kilometa moja na kuleta umeme hapa kwenye kisima hiki ni gharama kubwa kwa hiyo tuutunze mradi huu kwa maslahi mapana ya vijiji hivi,” amesema Jafo.
Aidha, Dk Jafo amezitaka Kamati za Maji za vijiji vya Ng’ambi na Mbugani ambako amezindua visima vya maji kuusimamia mradi huo ili uwe endelevu na kuleta faida kwa wananchi.
“Inawezekana baadae mkaongeza na tanki lingine kutoka hili moja lililopo kulingana na maelekezo ya wataalamu hivyo mtakuwa mmewezesha kupanua zaidi huduma hii na sisi kama Ofisi ya Makamu wa Rais tumetimiza jukumu letu la kuwasaidia wananchi kupambana na athari za mabadiiko ya tabianchi,” ameongeza Jafo.