WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo ameishauri Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuendelea kutoa huduma za hali ya hewa zilizo bora na zinazokidhi matarajio ya wadau , wakulima na wawekezaji.
Lengo ni kuweza kuchangia katika azma ya serikali ya awamu ya sita ya kuleta maendeleo endelevu kwenye sekta mbalimbali nchini.
Dk Jafo alisema hayo alipotembelea maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi ya Nanenane 2023 ya Kanda ya Mashariki inayojumuisha mikoa ya Pwani, Tanga, Dae es Salaam na Morogoro katika uwanja wa Mwalimu Nyerere, Morogoro.
“ TMA inafanya kazi kubwa sana , hivyo ninaiomba pamoja na kuwezeshwa na serikali ni vyema utaalamu uongezwe eneo la utabiri wa hali ya hewa uwe ni wa uhakika na wale wanaosajili miradi mikubwa ya uwekezaji watumie data za utabiri wa hali ya hewa. ” alisema Dk Jafo
Waziri Dk Jafo alisema wakulima nchini wanategemea kilimo cha mvua , hivyo utabiri wa hali ya hewa kwa wakulima na kwa wawekezaji ni jambo muhimu zaidi kwa maendeleo ya Taifa .
Alisema, kilimo kinahama zaidi kwani kile kilimo cha chakula kinabadilika na kuwa kilimo cha biashara zaidi.
Waziri Dk Jafo alisema kilimo cha biashara kitawezeshwa zaidi kwa kuwa na rasilimali za kutosha na vitendea kazi vya kutosha na utaalamu zaidi.
“Nilichokiona kwenye haya maonesho ya Kanda hii (Morogoro) kinalingana na makusudio ya Mheshimiwa Rais wetu Dk Samia Suluhu Hassan …sasa ombi langu kubwa ni kwa Watanzania wote lazima tutunze Mazingira “ alisema Dk Jafo
Kuhusu Mazingira, Dk Jafo alisema watanzania waelewe ya kwamba ukame unapotokea kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanasababisha kilimo chetu kinachotengemea mvua kisiweze kupata manufaa makubwa .
Alisema kuwa hali hiyo ipo kwenye upande wa maji, kwani endapo mito itashindwa kutiririsha maji , mifumo ya umwagiliaji haitafikiwa katika malengo yaliyokusudiwa na serikali.
Dk Jafo alisema, eneo hilo kuna uwekezaji mkubwa wa zaidi ya Sh bilioni 214.6 ambazo zimeelekezwa kwa ajili ya utengenezaji wa malambo makubwa karibu 1144 nchini .
“ Bila ya kuwa na maji ya kutosha hatuwezi kuwa na kilimo cha umwagiliaji , hivyo tunakila sababu ya kutunza mazingira na watanzana ni vyema kuzilinda rasilimali zilizopo” alisema Dk Jafo
Kwa upande wake,Mtaalamu wa hali ya hewa ya kilimo , Mecklina Merchedes alisema taarifa za hali ya hewa ni moja kati ya taarifa muhimu sana katika shughuli nyingi nchini .
Mecklina alisema, taarifa hizo husaidia uendeshaji wa shughuli ambazo husababisha ufanisi nzuri katika kusaidia maendeeleo na ukuaji wa uchumi.