SERIKALI imesema Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar umeendelea kuwa imara katika kipindi hiki unapotimiza miaka 59 tangu kuasisiwa Aprili 26, 1964.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo amesema hayo bungeni Dodoma jana wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Dk Jafo alisema serikali inatambua kuwa Muungano ni Tunu ya Taifa na utambulisho wa Tanzania duniani hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kuulinda, kuudumisha na kuuenzi kwa kuwa ni jambo la kujivunia. Alilieleza Bunge kuwa hadi sasa hoja nne za Muungano zimepatiwa ufumbuzi katika mwaka huu wa fedha 2022/23.
Alizitaja hoja hizo ni pamoja na malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili, kodi ya mapato (PAYE) na kodi ya zuio.
Hoja nyingine zilizopatiwa ufumbuzi ni pamoja na mkataba wa mkopo wa fedha za mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume (Terminal III) na ongezeko la gharama za umeme kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwenda Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO).
“Malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili ilitokana na kuwepo kwa utofauti wa ukadiriaji wa viwango vya thamani za bidhaa na kodi ya forodha baina ya Tanzania Bara na Zanzibar inayosababisha wafanyabiashara kulipa kodi ya ziada kwa bidhaa zinazotoka Zanzibar kwenda katika soko la Tanzania Bara,” alisema Dk Jafo.
Aliongeza: “Ufumbuzi wa hoja hii ulipatikana baada ya kubainika kwamba, wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa Zanzibar kutoka nje ya nchi na kupeleka Tanzania Bara hulazimika kulipia tofauti ya kodi iliyoachwa kukusanywa Zanzibar kutokana na tofauti ya uthaminishaji wa bidhaa, hivyo suala hili haliwafanyi kulipa kodi mara mbili badala yake hulipa kodi inayostahili kulipwa kwa uthaminishaji uliofanyika Tanzania Bara.”
Pia alisema hoja nne za Muungano zinazoendelea kutafutiwa ufumbuzi ni mgawanyo wa mapato yatokanayo na hisa za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na faida ya Benki Kuu, mapendekezo ya Tume ya pamoja ya fedha, usajili wa vyombo vya moto na uingizaji wa sukari inayozalishwa Zanzibar katika soko la Tanzania Bara.
Dk Jafo alisema serikali zote mbili zina nia ya dhati kuhakikisha hoja za Muungano zilizopo na zitakazojitokeza zinashughulikiwa kwa ushirikiano kwa lengo la kuulinda na kuudumisha Muungano huo adhimu