Jaji akiri hali ngumu maadili sekta ya umma

KAMISHNA wa Maadili wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Sivangilwa Mwangesi amesema ukosefu wa maadili kwa sasa umezua kilio kila kona hapa nchini kuanzia watoto wadogo wa shule hadi viongozi wa umma na kuwataka wadau wote kushirikiana kukabiliana nalo.

Jaji Mwangesi alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa wahariri wa vyombo vya habari nchini ulioratibiwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuhusu kuelimishana na kujadili mambo muhimu kuhusu ofisi hiyo.

“Hakuna ubishi katika ukweli kwamba suala la ukosefu wa maadili limezua kilio katika kila kona ya nchi yetu, kuanzia watoto wadogo wa shule, vijana hadi viongozi ambao sisi ndio wanaotuhusu, suala la uadilifu ni suala adimu, tunaamini hili sio wadao wote tukishirikiana tutakabiliana nalo, sio letu pekee,” alisema Jaji Mwangesi.

Alisema maadili yanasimamiwa na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 pamoja na kanuni zake na kuwaomba wahariri wasaidie kuelimisha jamii misingi ya maadili na ili kuwa na viongozi bora.

Jaji Mwangesi alisema tasnia ya habari ndio jicho, sikio na mdomo wa jamii na kwamba majukumu ya taasisi hiyo yakieleweka vizuri kwa wanahabari watachakata vyema taarifa zinazowafikia kuhusu viongozi wa umma na wananchi wengine kwa kuzihoji, kudadisi na kuzipembua kwa mujibu wa sheria.

Alisema vyombo vya habari na taasisi hiyo wakishirikiana katika mapambano ya utovu wa maadili katika jamii yatasaidia kurekebisha mienendo ya watu na kupunguza tatizo hilo.

Akitoa mada kuhusu Ukuzaji Maadili, Katibu wa Idara ya Ukuzaji wa Maadili wa sekretarieti hiyo, Waziri Kipacha aliwataka wahariri kuwa waadilifu ili wapate ujasiri wa kuelimisha jamii kuwa na maadili.

“Ili tuwe mfano kwa wengine na sisi tuwe waadilifu, mfano tukifichua mambo yanayofanywa isivyo halali na watumishi wa umma na sisi tuhakikishe ni wasafi ili jamii inaposoma habari hizo isihoji maswali ya uadilifu wako,” alisema Kipacha.

Alisema maendeleo ya sasa duniani yakiwemo ya teknolojia na utandawazi yamesababisha jamii kuwa na mwingiliano mkubwa wa mila, tamaduni na kuitaka jamii ya Kitanzania kuendelea kutunza tamaduni zao na kuacha kuiga za kigeni ambazo hazina misingi mizuri ya maadili.

Aliwataka wananchi kutoa taarifa za mienendo mibaya kwa viongozi pindi wawaonapo wakifanya katika jamii na kwamba sheria inamlinda mtoa taarifa hivyo wasiogope.

Kuhusu kiwango cha maadili cha sasa kwa viongozi wa umma, taasisi hiyo ilisema bado utafiti wa karibuni haujafanywa ili kuja na takwimu halisi lakini kwa utafiti wa mwaka 2016, ulionesha kiwango cha maadili kwa kundi hilo kiko asilimia 50.

Hata hivyo, walisema wako kwenye mchakato wa kutafuta fedha kwa ajili ya  kufanya utafiti kuhusu kiwango cha maadili kwa viongozi wa umma nchini.

Akizungumza katika mkutano huo, mmoja wa wahariri kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena alisema mkutano huo umekuwa jambo jema kwa sababu unawaleta pamoja na taasisi hiyo na vyombo vya habari na kuona jinsi ya kushirikiana katika kujenga misingi ya maadili kwa jamii.

Habari Zifananazo

Back to top button