Jaji kiongozi mstaafu atoa pendekezo uteuzi majaji

JAJI Kiongozi mstaafu, Amir Manento amependekeza uteuzi wa majaji unaofanywa na Rais uzingatie majina yaliyopendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama na si kutoka nje ya hao.

Jaji Manento amesema tume hiyo huchukua majina ya mahakimu, mawakili na watu wengine waliofanya kazi za sheria zaidi ya miaka 10 na kuchunguza kama wana sifa kuwa majaji wa Mahakama Kuu na Rufani.

Alisema hayo Dar es Salaam jana baada ya kuwasilisha mapendekezo hayo mbele ya Tume ya kuangalia jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai nchini. Manento ambaye pia ni Mwenyekiti mstaafu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora alisema ili haki itendeke na ionekane imetendeka, uteuzi wa majaji unapaswa kuwa ndani ya wale walipitishwa na tume kwani hufanya kazi zao kitaalamu.

“Miongoni mwa vigezo vinavyozingatiwa kuchagua majaji ni pamoja na uwezo wa kuandika hukumu, mwonekano mbele ya watu, lugha unayotumia na heshima yako ndipo tuna-recommend uwe jaji, haki haitendeki pale ambapo uteuzi utakuwa nje ya mapendekezo,” alisema.

Manento alisema Jaji Mkuu ndiye anayeomba kuruhusiwa kupata majaji baada ya kueleza kuna uhaba na ndiye mwenyekiti wa tume hiyo hivyo anapopeleka majina 30 huku uhitaji ni majaji 15, Rais ana uhuru mpana wa kuteua kati ya waliochujwa na wataalamu wa kisheria.

“Sifa ya kufanya kazi za sheria miaka 10 ni moja ya sifa ya kuwa jaji, sasa hatari ni pale ambapo umeshamteua kuwa jaji na wakati huohuo ni mwanasiasa nguli hivyo ni lazima atavuruga mhimili,” alisema.

Aidha, Manento alishauri kuwepo kwa chombo kitakachosimamia Jeshi la Polisi kitakachokuwa chini ya mahakama ili kuratibu na kuangalia makosa yanayofanywa na kusababisha kuvurugwa kwa mfumo wa haki jinai. Vilevile, alipendekeza serikali iwe na bajeti kwa ajili ya mashahidi kusaidia kuwezesha watu kutoa ushahidi bila vikwazo.

Habari Zifananazo

Back to top button