Jaji Mahakama Kuu atupa pingamizi kesi ya Sabaya
JAJI wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Salma Maghimbi, leo Desemba 14, 2022, ametupilia mbali pingamizi lililowekwa na mawakili wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro Lengai Ole Sabaya (35) na wenzake watano la kudai kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP), amekata Rufaa nje ya muda, ambapo Jaji huyo amesema hoja hiyo sio sahihi kwani rufaa imekatwa ndani ya muda.
Pia Jaji Maghimbi amesema hoja ya pili ya jopo la mawakili wa Sabaya, wakiongozwa na Mosses Mahuna kuwa taarifa ya kusudio la kukataa rufaa na sababu za rufaa zinatofautiana na idadi ya wakatiwa rufaa, haina msingi kwa kuwa haiwezi kuathiri mwenendo wa kesi, hivyo hoja hiyo inatupiliwa mbali.
Kutokana na hali hiyo Jaji Maghimbi alitoa muda wa dakika 15, kwa Mawakili wa Serikali na Mawakili wa Sabaya kujipanga, ili rufaa iweze kusikilizwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.



