‘Jamii ikemee usafirishaji haramu binadamu’

‘Jamii ikemee usafirishaji haramu binadamu’

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa ameitaka jamii kupigia kelele suala la usafirishaji haramu wa binadamu, ikiwa ni njia mojawapo ya kuidhibiti hapa nchini.

Alitoa rai hiyo Jumanne wakati akifungua warsha ya siku nne ya kuwajengea uwezo wasimamizi wa sheria kukabiliana na biashara haramu ya usafirishaji binadamu.

Warsha ilishirikisha maofisa wa polisi, waendesha mashitaka wa serikali, mahakimu, maofisa uhamiaji na maofisa ustawi wa jamii wa Mkoa Singida kwa ufadhili wa ubalozi wa Canada nchini.

Advertisement

Kamanda Mutabihirwa alisema biashara hiyo inayodhalilisha utu wa mtu imekuwa ikiendelea kwa muda mrefu huku waathirika wakubwa wakiwa ni wanawake na watoto. Alisema baadhi ya watu katika jamii, wakiwemo ndugu, wamekuwa wakisaidia kufanikisha mipango hiyo.

“Baadhi yetu, kwa kujua au kutojua, tumekuwa tukisaidia katika biashara hii. Sasa muda umefika tuanze kufikiria utu wa binadamu… tunapoona au kusikia vitendo hivi vikifanyika, tupige kelele kwa nguvu zetu zote ili suala hili likome kabisa,” alisema na kuongeza:

“Baada ya kupatiwa elimu hii nawasihi kila mmoja wenu akatende haki kwenye eneo lake na mshirikiane ipasavyo ili kutokomeza biashara hii nchini mwetu.”

Ofisa Mwandamizi Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji haramu wa Binadamu katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ahmad Mwendadi aliwataka wananchi, kuacha kudanganyika kuwa kwenda kufanya kazi nje ya nchi kuna maslahi mazuri.

Badala yake aliwataka watumie fursa zilizopo nchini kupambana kuinua uchumi wao kwa kuwa nje ya nchi wakati mwingine huweza kukumbana na madhila.

Alisema ili kukomesha uhalifu huo, serikali imeshawasilisha bungeni muswada wa kufanya marekebisho ya sheria hiyo kwa kuweka adhabu kali zaidi kwa mtu atakayepatikana na hatia ya kufanya biashara ya usafirishaji haramu wa binadamu.

Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Singida, Phaustine Ngunge alisema biashara hiyo haramu imekuwa ikichangiwa kwa kiasi kikubwa na wazazi wenyewe kutokana na umasikini. Pia inachangiwa na tamaa ya kusafiri nje ya nchi hususani kwa wenye umri wa miaka 15 hadi 30.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Tanzania Relief Initiative, Edwin Mugambila alisema kutokana na utafiti uliofanyika kuhusiana na biashara hiyo haramu, shirika lake limelazimika kuanzisha warsha za aina hiyo kwa mikoa yote kwa kuwa hakuna mkoa ulio salama na hadi sasa bado mikoa mitano kufikiwa na elimu hiyo.