Jamii yahimizwa kupaza sauti vitendo vya ukatili

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu ameitaka jamii, wadau na kila mmoja kwa nafasi yake kupaza sauti dhidi ya vitendo vya ukatili ambavyo vimekuwa vikiendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

Dkt. Jingu ameyasema hayo Jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi wakati akifungua kikao cha Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu  Wakuu kuhusu  mafunzo ya Usawa wa Kijinsia na Tathimini ya Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), Jijini Dodoma.

Amesema licha ya mafanikio yaliyopo kufuatia juhudi  zinazofanywa kukabiliana na vitendo hivyo  lakini bado ukatili umeendelea kufanywa hivyo ipo haja ya kuwa na afua mbalimbali za kuwatetea manusura wa vitendo hivyo.

“MTAKUWWA lengo lake ni kutokomeza ukatili wa aina zote unaofanywa katika jamii zetu sasa ukatili bado upo hivyo tumekubaliana kila mmoja wetu awe kinara wa mabadiliko chanya kuhakikisha tunakuwa na malezi bora, afua za kuyalinda makundi yote,”amesema Dkt. Jingu.

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu akizungumzia masuala ya ukatili

Vilevile ametoa wito  kila kundi kwa nafasi yake  Wizara za Kisekta, Taasisi za Serikali, Mashirika ya Kimataifa, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Viongozi wa Dini, Wazee wa Kimila na Vyombo vya Habari yana sehemu ya kufanya kwa kuongeza  juhudi za kuimarisha usawa wa jinsia na kutokomeza ukatili .

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake  na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula amewataka maafisa maendeleo kupitia ngazi ya Vijiji, Kata hadi Wilaya kutimiza wajibu wao kuhakikisha maendeleo yanapatikana, wananchi wanakuza  uchumi wao na kushiriki katika maendeleo kwa kulipa kodi.

 

“Kupitia mafunzo haya tumeongea mambo mengi yakiwemo mpango wa Kitaifa wa malezi kwa makundi ya vijana balehe ambao una malengo mengi kama kuzuia UKIMWI, mimba za utotoni, ajira na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kumuandaa mtoto kuwa kiongozi bora kuanzia ndani ya familia,”amebainisha Dkt. Zainab.

Aidha Mratibu wa MTAKUWWA, Joel Mangi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake  na Makundi Maalum ameeleza kuwa tangu kuanza kwa mpango huo mwaka 2017/18 na 2021/2022  umekamilika na kufanyika kwa tathmini ambayo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa ikiwemo kuongezeka kwa uelewa ndani ya jamii, uanzishwaji wa vituo 21 vya huduma kwa manusura wa ukatili ambapo vinafanya kazi nchi nzima.

Habari Zifananazo

Back to top button