Jamii yatakiwa kufufua ndoto za walemavu

WADAU wa mtoto mkoani Iringa wameilamu jamii wakisema ndiyo inayotengeneza mazingira ya watoto wenye ulemavu kutojiweza na kukosa fursa za maisha yaliyo jumuishi.

Lawama hizo walizosema zinapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa ili kuleta suluhisho ya changamoto za maisha jumuishi kwa watoto hao zilitolewa kwenye mdahalo uliondaliwa na Makutano TV na Rounding hands kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Iringa katika kuelekea kilele cha siku ya Mtoto wa Afrika.

Lengo la mdahalo huo lilikuwa ni kuchagiza malezi jumuishi na kukuza uelewa wa jamii juu ya umuhimu wa maisha jumuishi kwa watoto wenye ulemavu.

Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Iringa, Martine Chuwa alisema mazingira hayo ndiyo yanayosababisha watoto  wenye ulemavu kukosa fursa wanazostahili na hivyo ndoto zao za kimaisha kupotea.

Katika kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata ujumuishi alisema mkoa wa Iringa umeendela kutekeleza mipango mbalimbali inayolilenga kundi hilo ikiwemo utambuzi wa mapema, elimu, afya na uboreshaji wa miundombinu yao.

Akitoa takwimu za watoto wenye ulemavu Chuwa alisema mkoa wa Iringa una watoto 549 wanaoishi na ulemavu ukiwemo ulemavu wa viungo, Kutokuona, ukiziwi, akili na albino.

Akitaja sababu za kuwaleta wadau wa mtoto kwa pamoja katika mdahalo huo, Jesica Mwalyoyo wa Rounding Hands alisema mbali na maisha jumuishi kwa watoto wenye ulemavu kutoridhisha lakini pia wamekuwa wakisahaulika katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika.

Alisema watoto wenye ulemavu wanapitia changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kukataliwa, kufungiwa ndani, kukosa mahitaji yao ya msingi vikiwemo vifaa saidizi, na kukosa haki za kuabudu na kuchangamana katika matukio ya wazi ya kijamii na hata michezo.

Nao baaadhi ya wadau waliopata nafasi ya kuchangia katika mdahalo huo kwa pamoja wameona ipo haja  ya wataalamu kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili watoto hao waweze  kufikia ndoto zao kama watoto wengine wasio na ulemavu.

Aidha mmoja wa walemavu, Jema Mdegella ambaye kitaaluma ni mhasibu alitoa ushuhuda jinsi ilivyokuwa ngumu kwa jamii kumpokea hasa ilipofika wakati wa kwenda shule.

“Shule ilikuwa mbali, licha ya kuwa nina miguu yangu yote lakini kuna wakati ilinilazimu nitumie kiti mwendo ili kufika shuleni na kuna wakati ilinibidi kukaa chini kupisha watu wanaonishangaa kimo changu. Hakika imenichukua muda mrefu sana jamii kunikubali na kuishi na mimi,” alisema.

Zawadi Msigala mwanafunzi wa  sheria wa Chuo Kikuu cha RUCU alisema ilimlazimu kulazimisha maisha jumuishi kwenye jamii yake pamoja na watoto wenzie kumkimbia kwasababu ya ulemavu wake.

“Wenzangu walikuwa wananikimbia kwasababu nilikua natembea kwa kusota lakini hata ulipofika muda wa kuanza shule wengi walinikataa. Nawashukuru sana wadau wa nyumba ali kunitia moyo na kunipokea na sasa jamii inanipokea,” alisema.

Mmoja wa wazazi, Rehema Ugulumu alisema alipopata mtoto mwenye ulemavu ilichukua muda kukubaliana na hali hiyo lakini baadae yeye na mume wake iliwalazimu kuikubali japo kwa ndugu ilikuwa changamoto.

“Wengine walidhani imesababishwa na ukoo wangu; kuna wakati nilijisikia vibaya kuhukumiwa katika hilo lakini sikukata tamaa, changamoto ni pale nilipotaka kutoka na mtoto katika mazingira ya wazi, miundo mbinu katika sehemu nyingi si rafiki kuwafanya watoto hawa kujumuika,” alisema.

Mwongozo wa taifa wa utambuzi wa mapema na afya stahiki kwa mtoto mwenye ulemavu  wa Septemba 2021 unaonyesha ulemavu unaweza kuzuiliwa kwa asilimia 80 lakini pia utambuzi wa mapema  wa ulemavu kwa mtoto  unaweza kupunguza makali na athari za ulemavu ukubwani.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x