Jamii yatakiwa kupambana na ukatili

JAMII imetakiwa kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, kuwajali wajane na yatima ikiwa ni njia moja wapo ya kuleta amani na usawa katika kusherehekea siku ya Pasaka.

Hayo yamesemwa leo Aprili 9, 2023 na Askofu Mkuu wa Kanisa la Mennonite Tanzania, Nelson Kisare katika ibada maalum ya kusherehekea siku ya pasaka, iliyofanyika katika kanisa hilo Upanga jijini Dar es Salaaam.

Alisema watanzania wanapaswa kutafakari kwa kina suala la ukatili pamoja na kupiga vita kwa nguvu zote, sambamba na hilo Askofu Kisare ametoa wito wa kuendelea kutoa elimu ya neno la Mungu ili kubaliana na changamoto hizo.

Akizungumzia suala na mmomonyoko wa maadili, askofu huyo alisema kanisa lake linapinga vikali suala la mapenzi ya jinsia moja  na kuitaka jamii kuungana kwa pamoja kutoa elimu ya dini katika mwendelezo wa kupinga suala hilo.

“Sisi kama kanisa hatuwezi kukubaliana na suala la mapenzi ya jinsia moja, tutapiga vita, kanisa langu litashirikiana na wadau wengine katika kutokomeza kabisa suala hili”.alisema Askofu Kisare.

Hata hivyo hakusita kutoa neno la siku ya Pasaka ambalo alieleza kuwa siku hii sio tu kwa ajili ya kula na kunywa bali waumini wa dini ya kikristo wanapaswa kujitakasa kwa kuacha maovu na kuachana na vishawishi vyote vinavyoashiria kuwaletea dhambi.

Katika hatua nyingine askofu huyo aligusia suala la rushwa na kueleza kuwa suala hilo halipaswi kufumbiwa macho na kwamba kila mwana jamii anayo haki ya kupinga kwa nguvu zote.

Aidha, aliupongeza uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitahada za kuhakikisha wanatokomeza suala la rushwa ambayo aliita kuwa ni adui wa haki na kwamba kwenye rushwa hakuna amani.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Kanisa la Mennonite Tanzania, Amos Masanja alisema kuwa katika kusherehekea siku ya Pasaka jamii haipaswi kufanya matendo kinyume na sheria za mungu, bali kwa pamoja waungane kutenda mema.

“Ninachotaka kusema ni kuwa tuungane kwa pamoja kusherehekea Pasaka kwa kutenda mema na sio vinginevyo huu ndo ujumbe wangu kwa leo”.alisema Masanja.

Habari Zifananazo

Back to top button