Janza akunwa na ubora wa Stars

KOCHA wa timu ya taifa ya soka ‘Taifa Stars’, Honour Janza amesema timu yake imeonesha ubora wa kushindana kiasi cha kumpa matumaini kwamba wanaweza kufanya vizuri kwenye michezo ijayo ya kufuzu fainali za Afrika.

Stars iliyokuwa Libya kwa ajili ya michezo miwili ya kirafiki ya kimataifa, ilishinda mchezo mmoja dhidi ya Uganda bao 1-0 na kupoteza mabao 2-1 dhidi ya Libya katika mchezo uliochezwa juzi.

Akizungumza baada ya mchezo dhidi ya Libya, Janza alisema safari yao imekuwa nzuri kwa kuwa kucheza michezo miwili kuna kitu wamejifunza cha kiufundi na atayachukua kwa ajili ya kuyarekebisha.

“Tumecheza michezo miwili, mmoja tumeshinda na mwingine tulitegemea tushinde au tutoke sare, lakini tumepoteza, ila wachezaji wangu wamecheza vizuri, wameonesha nidhamu ya mchezo na ushindani wa hali ya juu,” alisema.

“Tulipoongozwa na Libya bao 1-0, tulipambana na kafanikiwa kusawazisha,  vijana wangu walicheza kwa kasi na kufanikiwa kusawazisha, lakini bahati haikuwa yetu tukapoteza,” alisema.

Alisema Libya ni timu nzuri yenye kasi na kwamba kuna kitu wamejifunza ikiwemo mbinu, namna ya kutoa pasi, namna ya kupeleka mashambulizi na kasi atayafanyia kazi kufanya vizuri zaidi.

Kwa mujibu wa kocha huyo wa Zambia, kikosi chake kimeonesha kuwa kinaweza kushindana na timu yoyote kutokana na ubora waliouonesha.

Michezo hiyo miwili ilikuwa ni ya kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) na huenda Kocha Janza baada ya kukaa na wachezaji kwa wiki moja atakuwa amejua aina ya kikosi chake kijacho baada ya kuona kiwango cha kila mchezaji.

Stars ina michezo ya kufuzu fainali za Afrika na baadaye inatarajiwa kucheza na Uganda, mchezo wa Kundi F, kukiwa na timu nyingine za Niger na Algeria.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x