Japan kusaidia wakimbizi Kigoma

Wakimbizi wa Burundi wakumbushwa kurejea nyumbani

SERIKALI ya Japan imetoa Dola za Marekani 360,000 kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kwa ajili ya kuhudumia kambi ya wakimbizi waliotoka DRC waliopo kambi ya Nyarugusu mkoani Kigoma.

Hafla ya kusaini makubaliano hayo mapya baina ya UNHCR na Serikali ya Japani imefanyika katika makazi ya Balozi wa Japan nchini Tanzania, jijini Dar es Salaam leo Jumatatu, Februari 12, 20224,

Akizungumza Balozi wa Japan nchini Yashushi Misawa amesema kuwa Japan ni mmoja wa wafadhili wakubwa kwa mashirika ya kimataia ya hisani kama UNHCR na kwamba ina historia ya muda mrefu katika misaada kwa nchi nyingi kupitia mashirika hayo.

Advertisement

Balozi Misawa amesema kuwa Japan imeshatoa msaada wa Dola 500,000 kwa UNHCR Tanzania ukiwemo ulioteolewa mwaka uliopita na kwamba msaada wa uliotangazwa leo wa Dola 360,000 kutoa mahitaji muhimu na huduma ya maji, neti za kuzuia mbu, sabuni na hududma nyingine za kijamii kwa wakimbizi hao wapya wa DRC.

“Mchango huu kutoka Serikali ya Japan tunaoutangaza leo ni mdogo sana kulinganisha na mahitaji halisi.Hata hivi tunaahidi kuendelea kutoa msaada kwa shughuli za wakimbizi kadri itakvyowezekana”, amesema Balozi Misawa.

Amesema, katika miaka ya hivi karibuni imeibuka migogoro katika nchi nyingi duniani inayohitaji msaada wa haraka, na kwamba baadhi zimekuwa zikipewa ungalizi wa karibu na kuacha mingine gizani ukiwemo mgogoro wa DRC ambao unaonekana kama umesahaulika.

Aidha, ameishukuru Tanzania kwa kuendeleza ukarimu wa kuwahifadhi wakimbizi hao.

Nae, Mwakilishi wa UNHCR Nchini Tanzania, Mahoua Parums ametoa wito kwa kwa wadau na wahisani mbalimbali wa haki za binadamu kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji wanaopewa hifadhi nchini Tanzania ili kuunga mkono juhudi na ukarimu wa Tanzania katika kuwapa hifadhi.

Parums amesema mpaka sasa Tanzania inawahifadhi wakimbizi na wahamiaji wapatao 240,000 kutoka nchi za Burundi na DRC na kwamba kati yao 14,000 ni wakimbizi wapya ambao wameingia nchini kuanzia Januari 2023.

Parums ameishukru Tanzania kwa kujitoa kwake katika kuendelea kuwapokea na kuwahifadhi wakimbizi akisema kuna nchi nyingi ambazo ni tajiri lakini wakimbizi hawakubaliki.

“UNHCR inawashukuru sana watu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wamekuwa mfano wa kimataifa katika kupokea na kuhifadhi wakimbizi. Ni muhimu kuendelea kudumisha mshikamano kati ya wakimbizi na jamii zinazowapokea”, amesema na kuongeza

“Watu wanaendelea kuja kila siku kutoka DRC na wanahitaji msaada wetu. Kwa bahati mbaya hivi sasa tunavyozungumza mwitikio wa wakimbizi nchini Tanzania hauna ufadhili, kwa kuwa ni asilimia 37 tu ya raslimali mali zinazohitajika kuwasaidia na kuwalinda wakimbizi nchini umepokelewa”, amesema Parums na kuongeza:

“Tunahitaji mshimano zaidi na msaada kutoka kwa wabia na wafadhili wote. Tunahitaji kuchukua hatua kwa pamoja kuzuia migogoro, tunahitaji kuoka maisha.”

Amesema kuwa UNHCR pamoja na wabia wake imejitoa kuisaidia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa hifadhi, msaada na suluhisho kwa wakimbizi na wahamiaji nchini Tanzania na kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya hifadhi za wakimbizi hao.

Kuhusu mchango huo wa Japan, Parums amesema kuwa UNHCR inaipongeza Serikali ya Japan kwa mchango huo wa thamani na uliotolewa katika wakati muafaka, ambao utaiwezesha UNHCR kutoa ulinzi na mahitaji muhimu kwa watoto, wanawake na wanaume wa Congo kuishi masiha ya kiutu.

Kwa mujibu wa Parums, UNHCR inahitaji Dola za Marekani Milioni 8 ili kuweza kukidhi mahitaji ya wakimbizi kutoka DRC, na kwamba inaendelea kuziomba jumuiya za kimataifa kuchangia misaada ya kibinadamu kadiri mahitaji yanavyozidi kuongezeka.

/* */