DAR ES SALAAM; Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi amemuomba Balozi wa Japan nchini Tanzania, Yasushi Misawa kutoa fursa kwa wataalamu wa Muhimbili kupata mafunzo mbalimbali ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia.
Prof. Janabi ametoa ombi hilo wakati wa ziara ya Balozi, Yasushi Misawa ambapo ametembelea maeneo mbalimbali ya utoaji wa huduma ikiwemo Idara ya magonjwa ya dharura ,Idara ya Radiolojia, Wodi maalumu ya uangalizi wa watoto (PICU), chumba cha matibabu ya dharura kwa watoto pamoja na eneo linalojengwa jengo la wagonjwa wa kulipia.
Prof. Janabi amemueleza Balozi, Misawa kwamba katika dunia ya sasa mafunzo kwa wataalamu wa afya ni muhimu hasa katika uboreshaji wa huduma unaoenda sambamba na uanzishwaji wa huduma mpya za kibingwa na kibobezi kama hospitali ya taifa.
“MNH ina matawi mawili Upanga na Mloganzila kuna takribani ya watumishi 3200 kwa pande zote mbili, watalaamu hawa wanahitaji kuendelea kupatiwa mafunzo yatakayowawezesha kuleta mapinduzi chanya ya utoaji huduma katika sekta ya afya hasa ukizingatia hospitali hii ni kubwa hapa nchini na inapokea wagonjwa wengi,hivyo nitumie fursa hii kukuomba ikitokea nafasi za mafunzo watumishi wa Muhimbili wapewe kipaumbele “amefafanua Prof. Janabi
Kwa upande wake Misawa amempongeza Prof. Janabi kwa maboresho makubwa aliyoyafanya Muhimbili na kumuhakikishia kuwa yuko tayari kushirikiana na hospitali hiyo katika kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya.
Naye Mkuu wa Idara ya magonjwa ya dharura, Dk. Juma Mfinanga amemueleza Balozi kwamba katika chumba cha huduma ya dharura cha watoto Muhimbili kwa siku uhudumia watoto kati ya 50 hadi 70 na kwamba wakifikishwa hufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu kwa dharura.