Jela kwa kumbaka mtoto wake

MAHAKAMA ya Wilaya ya Iringa imemuhukumu kifungo cha miaka 30 jela Imani Mfilinge (46) baada ya kumkuta na hatia ya kumbaka mwanaye wa miaka 13.

Mfilinge ambaye ni mkulima na mkazi wa kijiji cha Isimani alitenda kosa hilo Oktoba 11, 2022 chumbani kwake kijijini kwake.

Alifumaniwa na mkewe aliyerudi nyumbani ghafla akitokea msibani jirani na nyumbani kwao wakati akiendelea na tendo hilo.

Advertisement

Katika tukio hilo mahakama ilielezwa kwamba baada ya mtoto huyo kurudi nyumbani akitokea shule, baba yake alimtishia kwa panga kabla ya kumvuta chumbani kwake na kufanya dhambi hiyo.

Baada ya kumaliza kufanya kitendo hicho mbele ya mkewe aliyekuwa akijaribu kumnusuru mwanae, Mfilinge alijinasibu kwa mkewe huyo kwamba amepata mke mwenzake.

Hata hivyo mkewe huyo aliamua kwenda kwa mtendaji wa kijiji na kutoa taarifa hiyo na ndipo taratibu za kumkamata mtuhumiwa zikafanyika.

Kesi hiyo ilikuwa na mashahidi watatu, mhanga ambaye ni mtoto, mama wa mtoto pamoja na daktari aliyethibitishwa kuingiliwa kwa mtoto huyo.

Upande wa Jamuhuri katika kesi hiyo iliyosikilizwa na Hakim Mkazi Mwandamizi Rehema Myagilo uliwakilishwa na mwendesha mashtaka wa Serikali Veneranda Masai.

Hata hivyo Mtuhumiwa Imani Mfilinge alipopewa nafasi ya kujitetea hakuwa na chochote cha kusema ndipo mahakama ikamuhukimu kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka mtoto wake huyo aliyekuwa darasa la sita wakati tukio hilo likitokea.