MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha, imemfunga kifungo cha maisha Thomas Gwandu (39), mkazi wa Mtaa wa Olkerian, Kata ya Olasiti Arusha baada ya kukutwa na hatia ya kumlawiti binti wa miaka sita kwa muda wa miaka miwili.
Akisoma hukumu hiyo leo katika mahakama hiyo, Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, Herieth Marando, alisema mtuhumiwa alitenda makosa hayo mara kwa mara katika kipindi cha mwaka 2019 hadi 2021 kwa kumuweka unyumba mtoto huyo kabla ya kugunduliwa na wazazi wake na majirani.
Hakimu Marando alisema Mahakama ilijiriridhisha pasipo shaka yoyote kwa mashahidi watatu upande wa Jamhuri, akiwemo daktari ambaye aliwasilisha kielelezo kilichothibitisha kuwa mtoto huyo alilawitiwa mara nyingi na kuharibiwa vibaya sehemu ya haja kubwa.
Pia alisema ushahidi wa mtoto mwenyewe ulieleza kuwa alikuwa akichukuliwa wakati akitoka shule kila mara, kwa muda wote huo na kwenda kulawitiwa nyumbani kwa mtuhumiwa, kwani walikuwa majirani kabla ya wazazi kugundua.
Mtuhumiwa alipopewa nafasi ya kujitetea kabla ya kusomewa hukumu, aliiomba Mahakama kumpunguzia adhabu kwa kuwa anategemewa na wazazi wake na kosa hilo ni la mara yake ya kwanza.