WAKATI taifa likiadhimisha miaka mitatu ya kifo cha aliyekuwa Rais hayati Dk John Magufuli, Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kupitia kitengo cha mitandao imefanya mahojiano na Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali Venance Mabeyo na kueleza namna alivyokuwa bega kwa bega katika matibabu ya kiongozi huyo.
Usiku wa Machi 17, 2021 aliyekuwa Makamu wa Rais kwa kipindi hicho, ambaye ni Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza kifo cha kiongozi huyo kilichotokana na maradhi ya moyo akiwa katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam.
Dailynews Digital imezungumza na Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali Venance Mabeyo ameeleza siku moja kabla ya kifo cha hayati Rais Dk John Magufuli hali yake ilibadilika na aliomba arudishwe nyumbani.
Mstaafu Mabeyo anasema hayo katika mahojiano na mtandao wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali wa Dailynews Digital ambapo Mabeyo hakukubaliana na ombi hilo.
“Niseme jambo moja ambalo halikuwahi kusemwa huko nyuma kwa sababu nilikuwepo pale aliniita CDF (Mkuu wa Majeshi) njoo akaniambia siwezi kupona, waamuru hawa madaktari wanirudishe nyumbani nikamwambia mheshimiwa sina mamlaka hayo, akasema yaani CDF unashindwa kuwaamuru madaktari wanirudishe nyumbani,”? anasema Mabeyo akimnukuu baadhi ya kauli za hayati Magufuli.
Akizungumza na Dailynews Digital Mabeyo anasema alimwambia hayati Magufuli kuwa suala la afya siyo la Mkuu wa Majeshi hivyo alimuomba aendelee kubali hospitali chini ya uangalizi wa madaktari.
“Alipoona kwamba nimekuwa na msimamo huo akaniambia niitieni paroko wangu, Paroko wa St.Peters Father Makubi lakini akaongeza akasema namuomba Kadinali Pengo naye aje hiyo ni asubuhi sasa tukamtafuta Pengo alikuwa kwenye ibada hakupokea, akaniuliza CDF haujampata Pengo?
nikamwambia yuko kwenye ibada baba atakapotoka atakuja,” anaeleza Mabeyo.
Mstaafu huyo alisema baada ya hapo wote walikuja Kadinali Pengo na Father Makubi, anasema katika taratibu za kikatoliki wanamsalia ibada na kumpa sakramenti ya upako wa magonjwa aliyekuwa katika hatari ya kufariki”
“Walipomaliza kumsalia akapumzika lakini ilipofika saa nane mchana wakatupigia watu wa hospitali wakanipigia mimi kama Mkuu wa Majeshi, wakampigia DGIS na IGP wakatuambia hali ya mheshimiwa siyo nzuri sana hebu njooni, tukaenda tukamkuta ametulia lakini alikuwa hawezi kuongea tena, tukawaita madaktari wengine, nakumbuka tulimuita Profesa Maseru, Profesa Janabi alikuwepo muda wote kwa hiyo yule aliongezea nguvu wakajaribu kumuangalia, tukaendelea kukaa mpaka jioni, ikafika jioni saa kumi na mbili na nusu hivi au saa moja kasoro akakata roho,” anaeleza Mabeyo.