Jengo la dharura laokoa Sh milioni 56 Maswa

SIMIYU: Mganga mfawidhi Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu Dk James Bwire amesema kuwa baada ya serikali kujenga jengo la Huduma za Dharura katika hospitali hiyo, kiasi cha Sh milioni 56 kinaokolewa kila baada ya miezi mitatu.

Dk  Bwire amesema kuwa kabla ya jengo hilo kujengwa walitumia kiasi hicho kila baada ya miezi mitatu kwa ajili ya kusafirisha wagonjwa wa dharura kuwapeleka katika Hospitali ya Kanda Bugando jijini Mwanza.

Mganga mfawidhi huyo amesema hayo leo mbele ya Kamati ya kuhuduma ya Bunge ya Hesabu za serikali za Mitaa (LAAC), ambapo ameeleza mwaka 2020 walipokea fedha za Uviko -19 kutoka serikali kwa ajili ya kujenga jengo hilo.

Amewaeleza wabunge wa Kamati hiyo, ujenzi wa jengo hilo ulikamilika mwaka 2021 na Machi 2022 baada ya serikali kuleta vifaa vya kisasa lilianza kutumika ambapo mpaka Februari 29, 2024 wagonjwa 587 wamehudumiwa.

“Wagonjwa hao ni sawa na wagonjwa 54 kila mwezi, jengo hili lina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 20 kwa wakati mmoja, awali jengo lililokuwepo lilikuwa na uwezo wa kuhudumia mgonjwa mmoja kwa wakati mmoja,” amesema Dk Bwire.

Wabunge wa Kamati hiyo wamepongeza ujenzi wa jengo hilo, huku wakifurahi kujionea huduma nzuri ambazo zinatolewa kwa wagonjwa.

 

Habari Zifananazo

Back to top button