Jengo la magonjwa ya mlipuko lakamilika

SERIKALI imejenga jengo la magonjwa ya mlipuko eneo la Mwawaza mkoani Shinyanga kwa gharama ya Sh bilioni 1.9, fedha za Covid-19.

Imeelezwa kwamba jengo hilo limekamilika kwa asilimia 100 na sasa linasubiri vifaa kuanza kufanya kazi.

Mratibu wa Miundombinu ya afya Mkoa wa Shinyanga, Faustine Mulyutu alitoa maelezo hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Yudas Ndungile.

Mulyutu ambaye pia ni mtaalamu wa mionzi katika hospitali ya rufaa ya mkoa, alisema jengo hilo lina eneo la kutengenezea oksijeni kwani kipindi cha mlipuko wa virusi vya corona wagonjwa waliteseka na mitungi ilikuwa michache.

Alisema mradi huo wa kimkakati umejengwa kwa muungano wa wahandisi kutoka Chuo Kikuu cha Mbeya (MUST) kwa kutumia vifaa vya kutoka viwanda vya ndani.

“Jengo la magonjwa ya mlipuko litaweza kuhudumia watu wa hali ya chini takribani 40 na wale wenye kiwango cha juu (VIP) watu 12,” alisema.

Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mwaka wa uchaguzi mkuu 2020-2025 imebainisha magonjwa ya mlipuko na yanayosambaa kwa kasi kuwa hatari kwa maisha ya wananchi.

Ilani hiyo ilisema CCM itahakikisha nchi inakuwa na utayari wakati wote kwa kuzuia, kudhibiti na kukabiliana na majanga hayo kwa kushirikiana na wadau wengine.

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano 2021/22-2025/206 yanaeleza hatua muhimu zinazohusisha kuimarisha mifumo ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Habari Zifananazo

Back to top button