DAR ES SALAAM: Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema jengo la Timu ya Yanga si sehemu ya nyumba zitakazobomolewa katika mradi wa bonde la mto Msimbazi.
Akizungumza leo jijini Dar es salaam ameeleza kuwa nyumba zitakazobomolewa tayari wahusika walifahamishwa na wengine wamekwisha lipwa fidia, amewaondoa shaka mashabiki wa Yanga kuwa jengo la timu yao halipo kwenye orodha hiyo.
“Kufikia Februari 29 ,2024 TARURA ililipa fidia ya Sh bilioni 52.6 kwenye akaunti za wamiliki wa nyumba wapatao 2, 155 kati ya 2, 329 ambao walikuwa wameandikishwa kwenye daftari la kwanza, hivi sasa TARURA inakamilisha malipo ya fidia kwa wahusika wengine 446 waliomo kwenye daftari la pili” amesema Matinyi.
Ameongeza kuwa shughuli ya kubomoa nyumba hizo itaanza Aprili 15 mwaka huu na inatarajiwa kudumu kwa kipindi cha miezi mitatu hadi kukamilika kwake.
Aidha amesema maamuzi ya nyumba zitakazobomolewa yalifanyika baada ya tathimini za kitaalam na wahusika kufahamishwa faida za mradi huo huku akisitiza kuwa lengo ni kupunguza athari za mafuriko, matumizi bora ya ardhi pamoja na kupanua eneo la mto Msimbazi.