Jengo litakalobadili mandhari Arusha mbioni

Jengo refu kuliko yote katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini

ANGA la Arusha litabadilika hivi karibuni utakapokamilika ujenzi wa jengo refu kuliko yote katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini, ambalo linajengwa kwa ubia kati ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Umoja wa Posta Afrika (PAPU).

Jengo hilo pia litatumika kama Makao Makuu ya Papu.

Taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo iliyotolewa wakati wa ziara ya Bodi ya Wakurugenzi ya TCRA kwenye mradi huo mwishoni mwa wiki iliyopita inaonesha kuwa, ujenzi wa jengo hilo la ghorofa 19 umefikia asilimia 80.

Advertisement

Bodi ya TCRA ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Dk Jones Killimbe aliyeambatana na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari ilifanya ziara kwenye jengo hilo ili kujiridhisha na maendeleo ya ujenzi wake.

Jengo hilo litakuwa na huduma mbalimbali zikiwemo ofisi, maeneo ya biashara aina mbalimbali za kiwango cha kimataifa, ukumbi wa kisasa wenye viti vya kuhamishika kwa mfumo wa umeme na hoteli yenye hadhi ya utalii wa kimataifa.

Mpaka sasa linaendelea kutoa ajira na fursa nyingi kwa mamia ya wakazi wa Arusha na mikoa jirani.

Sifa nyingine ya jengo hilo imeelezwa kwamba mifumo mingi kwenye jengo itaendeshwa na kudhibitiwa kwa mifumo ya kielektroniki ili kutoa huduma kwa haraka na kwa ubora wa viwango vya kimataifa.

Ujenzi wa ghorofa hilo ni sehemu ya mkakati wa Papu inayoshughulikia masuala ya huduma za Posta barani Afrika kujitegemea kiuchumi katika uendeshaji, badala ya kutegemea michango ya kila mwaka ya nchi wanachama.