Jeshi la Polisi lamnasa mtuhumiwa wa mauaji Dar es Salaam

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia mfanyabiashara mmoja kwa tuhuma za kumuua Salum Ally aliyekuwa mlinzi wake ambae mwili wake ulikutwa Kibaha Misugusugu.

Kauli hii imetolewa  jana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam Muliro Jumanne Muliro wakati akielezea namna  Jeshi  la polisi lilivyojipanga kuhakikisha ulinzi na usalama kwa kipindi hichi cha sherehe za Christmas na mwaka mpya.

Muliro alisema Novemba 20, mwaka huu majira ya saa tano usiku polisi walipokea taarifa kuwa  Andron Mendez alifyatua risasi ndani ya yadi yake katika eneo la Tegeta Scansanca,Kinondoni.

Alisema baada ya tukio hilo zilipatikana taarifa za mtu mmoja kupotea na kutojulikana alipo,uchunguzi ulifanywa na kubaini kuwa mlinzi Ally hakuonekana tangu siku hiyo mpaka Desemba 2, mwaka huu alipokutwa Kibaha Misugusugu mwili wake ukiwa umetupwa na amefariki.

“Uchunguzi wa Jeshi la Polisi ulibaini Andron Mendez na wenzake kuhusika na tukio hilo la mauaji na kwenda kumtupa mlinzi huyo eneo alilokuwa,upelelezi unakamilishwa na watuhumiwa watafikishwa mahakamani haraka iwezekenavyo”alisema

Sambamba na hayo alisema kuelekea sherehe za mwaka mpya jeshi la polisi limejipanga kupambana na watu au vikundi vya uharifu vinavyopanga kufanya uharifu kipichi hiki na yoyote atakayehusika atashughulikiwa kwa mujibu sheria.

 

Habari Zifananazo

Back to top button