Bil 13/- zatengwa kuboresha Tazara

SERIKALI imesema katika mwaka wa fedha 2022/23, imetenga Sh bilioni 13.1 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya reli ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete amesema bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Njombe Mjini (CCM), Deodatus Mwanyika. Mwanyika alitaka kufahamu mkakati wa serikali wa kukarabati reli ya Tazara.

Mwakibete alisema serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuboresha miundombinu ya reli hiyo. Alisema katika mwaka wa fedha 2022/23, serikali imetenga Sh bilioni 13.1 kwa ajili ya ununuzi wa mataruma ya mbao kwa ajili ya kufanyia ukarabati madaraja 172 yaliyopo upande wa Tanzania.

Alisema pia ununuzi wa mtambo wa kisasa wa kushindilia kokoto kwenye reli na ununuzi wa mtambo wa kuvunjia kokoto kwa ajili ya kuongeza kokoto za aina mbalimbali zinazotumika katika kufanyia matengenezo ya njia ya reli kati ya Dar es Salaam –Tunduma na Msolwa – Kidatu.

Pia Mwakibete alisema fedha hizo pia zitatumika kukarabati mabehewa 21 ya treni za abiria za Udzungwa na treni za abiria za mjini za jijini Dar es Salaam. Kwa upande wa mikakati ya muda wa kati na mrefu, alisema serikali za Tanzania na Zambia zimeandaa Mpango wa Biashara wa miaka mitano ambao unatarajiwa kupitishwa na Baraza la Mawaziri mwishoni mwa Novemba, 2022.

Alisema pia serikali za Tanzania, Zambia na China zimeunda timu ya pamoja kwa ajili ya kuandaa mkakati wa pamoja kwa kuishirikisha Serikali ya Watu wa China katika kugharamia maboresho ya Tazara. Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inaeleza kuwa chama kinatambua kuwa uendelezaji wa miundombinu ya uchukuzi ni hitaji la msingi katika kuchochea na kuwezesha maendeleo ya sekta za kiuchumi na kijamii.

Katika ilani hiyo, CCM inaeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2015 – 2020) kiliielekeza serikali kuimarisha na kuboresha miundombinu na huduma za reli, bandari, viwanja vya ndege; kununua ndege, meli za abiria na mizigo; na kuboresha utabiri wa hali ya hewa. Lengo ni kuchochea ukuaji wa uchumi na kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button