MKUU wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee, ameagiza halmashauri zote mkoani humo kujifunza kwa Manispaa ya Musoma katika kuwezesha wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (Tasaf), kupokea malipo kwa njia ya mtandao (simu au benki).
Maagizo hayo yametokana na taarifa za utekelezaji wa mpango huo robo ya kwanza Julai – Septemba, za kila wilaya mkoani humo kuonesha wanufaika wengi wanapokea malipo hayo kwa fedha taslimu, ilhali muongozo unataka wote wapokee kwa mtandao.
Taarifa hizo zimewasilishwa na waratibu wa Tasaf wa kila wilaya, kwenye kikao cha mkoa huo kutathmini utekelezaji wa mpango huo, ambapo pamoja na mengine, imebainika kuwa Manispaa ya Musoma peke yake ndiyo inaongoza kwa kufanya vizuri katika eneo hilo.
“Manispaa ya Musoma ina asilimia 89 ya wanaolipwa kwa mtandao, wakati Butiama ina asilimia 1, Rorya asilimia 8, Tarime DC asilimia 12, Bunda DC asilimia 12, Bunda TC asilimia 18, Serengeti asilimia 20 na Tarime TC asilimia 28,” alisema.
Meja Jenerali Mzee ameelekeza wakurugenzi katika halmashauri hizo kushirikiana na wataalamu wanaohusika katika utekelezaji wa mpango huo, kutumia maofisa ustawi wa jamii na kubuni mbinu nyingine, ili kuwezesha kila mnufaika kupokea malipo hayo kwa mtandao.