IRINGA: SERIKALI imehadharisha umma dhidi ya dawa zinazotembezwa mkononi ikiwa ni pamoja na zinazouzwa katika vyombo vya usafiri kinyume na sheria kutokana na kuwapo ambazo ni duni na bandia.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba ametoa rai hiyo leo mjini Iringa kwenye ufunguzi wa kikao kazi kati ya wahariri wa habari kutoka vyombo mbalimbali na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).
“Wananchi waache mara moja kununua dawa zinazotembezwa mikononi ikiwa ni pamoja na katika vyombo vya usafiri kinyume cha sheria kwani mara zote dawa hizo huwa ni duni au bandia,” amesema Serukamba.
Ameongeza: “Serikali haitamwonea huruma mtu yeyote atakayepatikana na dawa bandia kwa kigezo kuwa hawakujua kwamba ni bandia wakati huo huo akiwa amesababisha madhara kwa wagonjwa.”
Ameomba wahariri wa habari kutumia vyombo vyao kuelimisha jamii ifahamu TMDA na kazi zake, iweze kutoa taarifa inapotilia mashaka ubora na usalama wa bidhaa za dawa na vifaatiba vilivyo sokoni.
Awali Mkurugenzi wa TMDA, Dk Adam Fimbo amesema mamlaka imefanikiwa kiasi kikubwa katika kufikia malengo yake kwa kuhakikisha kwamba jamii inakuwa salama kutokana matumizi ya dawa, vifaatiba, vitendanishi na bidhaa nyingine vinavyohusiana na afya.
Kwa mujibu wa Dk Fimbo, TMDA imefanikiwa kuweka na kuimarisha mifumo ya udhibiti wa bidhaa nchini ikiwamo mifumo ya tathmini na usajili wa bidhaa, ukaguzi wa viwanda na maeneo ya biashara, utoaji na uingizaji bidhaa, ufuatiliani wa usalama wa dawa pamoja na majaribio ya dawa.
Uboreshaji huo umeifanya mamlaka kufikia na kushika ngazi ya tatu ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kati ya nne kwa kuwa na mifumo bora ya udhibiti wa dawa hivyo kuwa taasisi ya kwanza ya udhibiti barani Afrika kufikia ngazi hiyo mwaka 2018.