HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeweka mkakati wa kukabiliana na ongezeko la wamachinga kwa kuanza kujenga masoko mengine ya kisasa kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema baada ya kukamilisha ujenzi wa soko la kisasa la wamachinga, jiji limejipanga kukabiliana na ongezeko la wafanyabiashara hao watakapokuwa wametosha kwenye soko hilo kuu la wazi.
“Tumejipanga kuhakikisha wanapojaa soko la wamachinga tunahamishia masoko madogo, hatutasubiri watuzidi nguvu tena, uwezo wa soko ni watu 5,000 wakifika 5,001 huyu tunampeleka kwenye masoko madogo, hawatatuotea tena,” alisema.
Mafuru alibainisha kuwa masoko madogo ambayo yameboreshwa ni Makole, Chang’ombe, Kikuyu Kusini, Tambukareli na Kisasa.
Alisema mbali na masoko madogo, pia jiji limepanga kujenga masoko makubwa ya wamachinga katika eneo la Mnada mpya njia ya kuelekea Singida na katikati ya Stendi ya mabasi ya kwenda mkoani na Soko Ndugai ambayo yako kwenye hatua ya usanifu.