Jina la Pele laingizwa kwenye kamusi Brazil
PELE, jina la utani la mfalme wa soka duniani ambaye aliaga dunia Desemba mwaka jana, rasmi limeingia kwenye kamusi ya Michaelis ambayo ni maarufu kwa lugha ya Kireno nchini Brazil likimaanisha ni ya ‘kipekee, isiyolinganishwa’.
Kujumuisha kwa jina hilo kwenye kamusi hiyo imekuja kama heshima baada ya kampeni ya taasisi ya Pele Foundation iliyotaka gwiji huyo kuenziwa na kukusanya waungaji mkono zaidi ya 125,000.
Mchezaji pekee kuwahi kushinda Kombe la Dunia mara tatu anachukuliwa kuwa mwanasoka bora wa muda wote katika historia ya mchezo wa soka.
Wakati wa maisha yake kama mwanasoka ambayo yalidumu kwa kipindi cha zaidi ya miongo miwili, aliweka rekodi ya kufunga mabao 1,281 katika klabu yake ya Santos, timu ya taifa ya Brazil na klabu ya New York Cosmos ya Marekani.
Tangu kifo chake kilichosababishwa na saratani ya koo, luninga ya klabu yake ya zamani ya Santos na taasisi ya Pele Foundation wamekuwa wakiendesha kampeni ya kutaka jina la staa huyo kuenziwa kwenye kamusi maarufu nchini humo.
Jumatano hii wachapaji wa kamusi ya Michaelis walitangaza jina hilo kuwa litajumuishwa kwenye misamiati ya kamusi hiyo mara moja na tayari toleo lijalo litakuwa na msamiati wa jina la utani la gwiji huyo wa soka.
Msamiati huo utasoma: “pe.lé kisifa likimaanisha mtu wa kipekee, mwenye thamani, bora na asioweza kulinganishwa na kitu chochote.
Taasisi ya Pele Foundation ilianzishwa kutunza heshima ya mfalme huyo wa soka na inayoendana aliyofanikiwa kama mwanasoka.