JK aipongeza JKCI kuipa heshima Tanzania

JK aipongeza JKCI kuipa heshima Tanzania

RAIS mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete ameipongeza Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuipa heshima Tanzania kwa kutoa misaada kwa Watanzania na kuokoa maisha ya watu wengi.

Dk Kikwete alisema hayo mwishoni mwa wiki Dar es Salaam wakati akikabidhi hundi ya shilingi milioni 100 zilizotolewa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kupitia mbio za TPDC Marathon msimu wa kwanza kwa ajili ya kuchangia tiba ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa kwenye taasisi hiyo.

Alisema upasuaji wa moyo una gharama kubwa na JKCI ndani ya miaka saba tangu kuanzishwa kwake imekuwa kituo cha ubingwa kinachotoa huduma za matibabu ya moyo kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Advertisement

“Tusingekuwa na Taasisi hii sina hakika wale wote ambao wameshapata matibabu JKCI wangekuwa sasa hivi wako katika hali gani, kwa sababu tangu kuanzishwa kwa Taasisi hii jumla ya wagonjwa wa moyo elfu saba na mia sita wameshafanyiwa upasuaji wa moyo,” alisema Dk Kikwete.

Aliongeza: “Tunaokoa maisha ya watu wengi na hadi sasa kuna watoto 511 wanaohitaji matibabu haya wapo kwenye foleni ya kusubiri huduma ya upasuaji wa moyo.”

Alisema awali Tanzania ililazimika kupeleka wagonjwa nje kwa matibabu na gharama yake ilikua dola elfu saba kwa kila mgonjwa hivyo ilikuwa ngumu kwa mtu wa kawaida kumudu.

Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Dk James Mataragio aliwashukuru waliojitokeza kuwaunga mkono kuwachangia watoto wenye magonjwa ya moyo.

“TPDC imekua ikijishughulisha na kufanya kazi na jamii mbalimbali ambazo zinatuzunguka kwa kuchangia katika masuala ya elimu, michezo na shughuli mbalimbali za kijamii lakini leo tumeona twende katika hatua nyingine ya kusaidia kuokoa maisha ya watoto wenye magonjwa ya moyo,” alisema Dk James.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi alisema kila mwaka Tanzania wanazaliwa watoto milioni mbili, asilimia 0.8 mpaka moja ya hao wanakuwa na matatizo ya moyo na katika hao asilimia 25 uhitaji upasuaji wa moyo.

“Kila mwaka tumekuwa tukifanya upasuaji wa moyo kwa watoto kati ya 250 na 300, kupitia mbio za TPDC Marathon watoto 50 wamechangiwa shilingi milioni 100 ambapo kila mtoto amechangiwa milioni mbili na fedha nyingine iliyobaki katika matibabu ya watoto hao itajaziwa na serikali,” alisema Profesa Janabi.