JK atamani makubwa zaidi Tanga School

DAR ES SALAAM; RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amesema anataka Tanga School iwe miongoni mwa shule zinazoshika nafasi ya juu hapa nchini.

Kikwete amesema hayo wakati wa uzinduzi wa umoja wa wanafunzi waliosoma katika shule hiyo kuanzia miaka ya 1960 hadi sasa uliofanyika mkoani Dar es Salaam.

” Tunataka Tanga School iingie kwenye shule moja yenye ufaulu wa juu. Tutakaa na uongozi wa shule, tujue nini tuchangie ili shule yetu hii iingie kwenye orodha hiyo,” amesema Kikwete.

Amesema shule hiyo ambayo kwa sasa inajulikana kama Tanga Technical School, alisoma hapo kidato cha tano na sita pia imetoa watu mashuhuri mbalimbali hapa nchini, ikiwa ni pamoja na wenye taaluma mbalimbali.

Amesema haitapendeza shule hiyo ambayo ni ya sekondari ya kwanza hapa nchini ipotee kwenye ramani ya elimu.

Amesema kupitia umoja waliouanzisha  wataiwezesha shule hiyo iwe na maktaba mtandao, vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na ubora wa elimu.

Awali Mwenyekiti wa umoja huo, Meja Jenerali Khamis Semfuko amesema haikuwa kazi rahisi kukusanya dhamira za waliosoma miaka ya 1960 na kuziunganisha na dhamira za vijana wa sasa waliopita shuleni hapo mpaka kufikia kuunda taasisi rasmi.

” Hatua hii inalenga kuboresha kiwango cha ufaulu pale Tanga School na ni chachu ya mageuzi makubwa ya maboresho ya miundombinu ya kuinua viwango vya taaluma kulingana na kasi ya teknolojia ya sasa,” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule, Mackmaster Mnondwa amesema kuwa atahakikisha shule hiyo inashika nafasi ya kumi bora kama umoja huo ulivyokusudia.

Amesema shule hiyo yenye wanafunzi 1126, kati ya hao wanawake ni 194, wanaume 932, kidato cha tano wako 279 na wenye mahitaji maalum 163.

Amesema mwaka jana ufaulu katika shule hiyo daraja la kwanza walikuwa 94, daraja la pili 42, daraja la tatu 27, la nne 28 na daraja O walikuwa 10.

Habari Zifananazo

Back to top button