JK: Samia amestahili PhD ya heshima

MKUU wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais Mstaafu, Dk Jakaya Kikwete amesema Rais Samia Suluhu Hassan alistahili kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari kutokana na sifa, vigezo na kazi alizofanya na anazofanya kuwatumikia wananchi.

Dk Kikwete alisema hayo jana kwenye Mahafali ya 52 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Alimtunuku Rais Samia shahada hiyo baada ya Bodi ya UDSM kumpendekeza na kuchambua wasifu wake na kazi alizofanya zilizokidhi vigezo vya kupewa tuzo hiyo.

“Kwa mamlaka niliyokabidhiwa, ninakutunuku Digrii ya Heshima ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hongera sana,” alisema Kikwete.

Advertisement

Alisema Baraza la UDSM lilikaa na kuchambua wasifu na kazi za Rais Samia na kutambua amekidhi vigezo vya tuzo hiyo kutokana na mchango wake katika jamii kielimi na kiuchumi kubadilisha maisha ya watu.

“Tumefurahi umekubali ombi letu na leo umeingia rasmi katika wanafamilia wa chuo chetu, karibu,” aliongeza Rais huyo wa Awamu ya Nne Tanzania.

Rais Samia alishukuru akisema ameipokea kwa unyenyekevu na ni heshima kwa Watanzania waliomuamini. Alisema aliitamani siku za nyuma ila alikosa muda wa kusoma kutokana na majukumu mengi ya kitaifa.

“Nimeipokea tuzo hii kwa unyenyekevu mkubwa, nilijiuliza maswali kadhaa sababu huko nyuma nilijaribu kuitafuta shahada hii lakini nikakosa muda,” alisema Rais Samia.

Alisema kutunukiwa kwake shahada hiyo kunamwongezea chachu ya kuwatumikia vizuri zaidi wananchi na kusema hiyo ni dhamana kubwa aliyopata pia kwa kutumikia serikali zilizopita.

Januari 27, mwaka huu wakati akisherehekea siku yake ya kuzaliwa, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), lilifanya mahojiano maalumu kutoka Ikulu Chamwino, Dodoma na Rais Samia alisema alijaribu kufanya Shahada ya Uzamivu (PhD), lakini kutokana na majukumu mengi alishindwa na kusema angeimalizia baadaye.

Alieleza safari yake ya elimu na masuala mengine aliyopitia hadi kushika wadhifa wa juu wa uongozi wa nchi, na kubainisha kuwa katika safari yake ya elimu ameishia kwenye Shahada ya Uzamili na alikuwa na nia ya kufanya PhD, lakini majukumu yamembana.

“Nilijaribu kufanya PhD lakini ukweli ni kwamba pilika ni nyingi nimeshindwa, sijui niseme nimeshindwa au nitaimalizia baadaye, sijui. Labda nitaimalizia baadaye,” alisema Rais Samia mapema mwaka huu.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *