JKCI kuendesha matibabu ya moyo Geita

TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), inatarajia kufanya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato, iliyopo Mkoa wa Geita.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano, Anna Nkinda, imesema kuwa wataalmu wa JKCI watashirikiana na wataalamu wa hospitali ya hiyo kuhudumia wananchi.

Amesema upimaji huo utafanyika kwa watoto na watu wazima  kuanzia leo Oktoba 13  hadi Novemba 4, 2022 kuanzia saa mbili kamili asubuhi hadi saa 10 jioni  katika viwanja vya hospitali hiyo.

“Tutakuwa na wataalamu wa lishe, ambao watatoa elimu ya lishe bora ambayo itawapa wananchi uelewa na kufuata mtindo bora wa maisha, utakaowasaidia kuepuka  magonjwa ya moyo,”ameeleza Nkinda.

Amebainisha kuwa watakaogundulika  kuwa na matatizo  ya moyo watafanyiwa uchunguzi zaidi  na kupatiwa matibabu hapohapo  au kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI.

Amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao, kujua kama wana matatizo ya moyo, ili kuanza matibabu mapema  kwa watakaobainika kuwa na tatizo.

“Kwa taarifa zaidi wasiliana kwa namba 0655345566 na Dk Gerald Muniko na  kwa namba 0765939068 Fadhila Mwambene,”amesisitiza Nkinda.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x