JKCI kupokea wagonjwa kutoka Zambia, Rwanda

TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam leo imesaini mikataba na nchi mbili za Rwanda na Zambia kwaajili ya kupokea wagonjwa wa moyo kutoka nchi hizo na kutoa mafunzo kwa wataalamu.

Hatua hivyo imekuja mara baada ya JKCI kuwa kituo bora cha matibabu ya moyo barani Afrika ambapo wagonjwa kutoka nchi mbalimbali hutibiwa hapo.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba hiyo,Mkurugenzi wa JKCI, DK Peter Kisenge amesema kwa mwezi mmoja wanapokea wagonjwa takribani 20 kutoka nchi mbalimbali.

“Siku ya leo tumefanya tukio kubwa la kusaini mikataba kwa lengo la kubadilisha matibabu kwa nchi za wenzetu Rwanda na Zambia kuweza kuleta wagonjwa hapa na kuwatibu na kwaajili kuwafundisha wataalamu wa afya katika nchi zao ili waweze kutoa huduma.

“Takwimu za mwaka jana tulihudumia wagonjwa 150,000 ambapo kati yao wagonjwa 600 walifanyiwa upasuaji mkubwa na upasuaji mdogo walikuwa 1,456.

Amesema Wagonjwa hao wa nje 20 walitoka nchi za Malawi,Visiwa vya Comoro, Kenya, Uganda, Zimbabwe, Zambia, Rwanda na Burundi.

“Pia tulipata wagonjwa wanaotoka Ulaya wanakuja kwaajili ya utalii wakipata tatizo wanakuja tumepata kutoka Norway,Uingereza,India na Polanda sio tu Afrika tunahudumia duniani nzima,”ameeleza Dk Kisenge.

Amesema kutokana na kuimarika kwa huduma za moyo nchi sasa wanaopata rufaa za kutibuwa nje ya nchi ni asilimia mbili tu.

Dk Kisenge amesema Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika rasilimali watu na miundombinu na imefanya kuwa taasisi kubwa inayoongoza Afrika kwa matibabu ya moyo.

“JKCI inaendelea kutoa huduma mikoa mbalimbali kwa kuwa karibu na wananchi na sasa pia tunaenda kusaidia nchi zingine,”ameeleza.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya,Naibu Katibu Mkuu,Dk Grace Maghembe amesema uwepo wa mikataba hiyi ni matunda ya uwekezaji uliofanywa na serikali katika taasisi hiyo.

“Tunamshukuru Rais Samia katika kufanikisha utiaji saini tumefika hali sasa JKCI imekuwa kubwa kiasi kwamba ndani ya Afrika wenzetu wamekuja kusaini mikataba huu ili wawalete wagonjwa wao hapa.

Habari Zifananazo

Back to top button