JKCI kutoa huduma bure Namtumbo

DAR ES SALAAM; TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kwa kushirikiana na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, wanatarajia kufanya kambi maalum ya matibabu kwa siku saba bure katika Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, ili kupeleka huduma karibu ya wananchi.

Hadi sasa JKCI imefanya huduma za tiba mkoba ijulikanayo kama Dk Samia Suluhu Outreach Service kwa mikoa 16, ambapo wananchi 16,000 walijitokeza kupima afya zao, huku asilimia 25 walikutwa na shikizo la juu la damu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa JKCI, Dk Peter Kisenge,  amesema kambi hiyo itaanza Julai 8 hadi 13, 2024, kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 10 jioni katika kituo cha afya Lusewa na Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/matibabu-ya-moyo-kufanyika-mikoani/

“Kutakuwa na wataalamu wa lishe ambao watatoa elimu ya lishe bora itakayowapa wananchi uelewa na kufuata mtindo bora wa maisha utakaowasaidia kuepuka magonjwa ya moyo yanaweza kuepukika kwa kufuata ushauri wa kitaalamu,” amesema.

Amesema watakaogundulika kuwa na matatizo ya moyo watafanyiwa uchunguzi zaidi na kupatiwa matibabu hapo hapo au kupewa rufaa ya kuja kutibiwa JKCI.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Namtumbo, Vita Kawawa amesema wanawatangazia kuwa Wilaya ya Namtumbo na Mkoa wa Ruvuma nao wamepata fursa ya kufikiwa na tiba mkoba kwa kupimwa magonjwa ya moyo kwa siku saba.

“Watakuwa katika Hospitali ya Wilaya na kutoa mafunzo ya lishe madaktari wetu kule kwa sababu tuna mashine za ECG na ECO watajifunza,” amesema

Amewataka wananchi wote kujitokeza kupima afya zao na kupata matibabu bure kwani matibabu yoteyamelipiwa na Rais Samia.

Naye Mkuu wa Divisheni ya afya ustawi wa jamii na huduma za lishe ,Dk Aaron Hyera amesema mbunge wa jimbo hilo amefanya maendeleo mengi na anatoa ushirikiano mkubwa, ambapo sasa serikali imejenga hospitali mpya ya wilaya ambayo ilijengwa kwa Sh bilioni 4.2 na itaenda kutumika kutoa huduma.

“Kuna vituo vipya vya afya ambavyo vilijengwa kwa Sh bilioni 2 na tunawakaribisha madaktari wanaokuja kutoa huduma za kibingwa na madaktari wetu watashiriki kupata utaalamu na kuendelea na hizo huduma,” amesema.

 

Habari Zifananazo

Back to top button