JKCI kutoa matibabu ya moyo Kisarawe
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI) kesho itaanza kufanya kambi ya matibabu itakayohusisha upimaji na matibabu ya moyo kwa wananchi Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani.
Kambi hiyo ya matatibabu inatararajiwa kuanza Mei 17 hadi 19, 2023 kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa 12 jioni Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano, Anna Nkinda imesema wagonjwa watakaogundulika kuwa na matatizo ya moyo watafanyiwa uchunguzi zaidi na kupatiwa matibabu hapo hapo au kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi hiyo.
“Wataalamu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe iliyopo Pwani watafanya upimaji na matibabu ya moyo kwa wananchi,”ameeleza.
Amewaomba wananchi wa maeneo hayo na mikoa ya jirani wajitokeze kwa wingi kupima afya zao kujua kama wana matatizo ya moyo, ili kuanza matibabu mapema kwa atakayebainika kuwa mgonjwa .
“Kwa taarifa zaidi wasiliana na Dk Zaituni Hamza Mganga Mkuu Kisarawe kwa namba 0717949477 na Dk Yona Kabata ,Mganga Mfawidhi wa kisarawe,” imesema taarifa hiyo.