JKCI yaokoa bil 31.1/- wagonjwa kutibiwa nje

TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imedhamiria kuimarisha tiba za moyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo kwa kutoa huduma ya kupandikiza moyo.

Pia Mkurugenzi Mkuu wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema Dar es Salaam kuwa kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2022/23 serikali iliokoa Sh bilioni 31.1 ambazo zingelipwa kama wagonjwa wangetibiwa nje ya nchi. Dk Kisenge alisema hayo wakati anatoa taarifa kuhusu malengo na mafanikio ya taasisi hiyo.

Kuhusu kupandikiza moyo alisema moyo ukichoka kufanya kazi unabadilishwa ukitoka kwa aliyejitolea. Alitoa mfano kuwa inawezekana yupo aliyepata ajali mbaya na si rahisi kupona, hivyo moyo wake unaweza kuchukuliwa na kuwekwa kwenye chombo ili utumike.

“Hapa nimesema hayo ni maandalizi ya taasisi hii kufikia huko kwa miaka ijayo, inaweza kuwa mitano ama sita kwani lazima zipo taratibu mbalimbali zitakazowezesha kufikiwa huduma hii,” alisema Dk Kisenge.

Alisema kufikia Oktoba mwaka huu wanafikiria kuanza huduma ya kubadilisha valvu za moyo bila kupasua kifua na kwamba kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki itakuwa taasisi pekee inayotoa huduma hiyo.

Alisema huduma inaweza kufanyika kwa kuwa imegundulika njia ya kutumia mirija na kupitishwa kwenye eneo la mwili kama kuwekewa tundu dogo kwenye paja na kuelekezwa hadi kwenye moyo na mashine kuelekeza namna ya kubadilisha valvu za moyo.

“Huduma hii inaweza kufanywa zaidi kwa wagonjwa wa kisukari na saratani ili kutopasua vifua,” alisema Dk Kisenge.

Alisema katika mwaka wa fedha 2023/24, JKCI itazidi kuimarisha huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo kwa kuwa wataalamu wanazidi kuongeza ujuzi.

Dk Kisenge alisema kukamilika jengo la utawala na vipimo lililogharimu Sh bilioni 3.6 kutasaidia wagonjwa wengi zaidi kupata huduma za vipimo vya moyo ndani ya saa mbili. Jengo hilo linatarajiwa kukabidhiwa Agosti mwaka huu.

Alisema wataendelea kusogeza huduma za matibabu ya kibingwa ya moyo kwa wananchi kwa kuwafuata walipo.

“Tunafanya hivi kwa kuwa asilimia kubwa ya wagonjwa tunaowatibu mioyo yao huwa imechoka, hii ni kutokana na kuchelewa kufika JKCI kwa ajili ya kupata matibabu ya kibingwa ya magonjwa haya,” alisema Dk Kisenge.

Alisema kwa mwaka 2022/23, JKCI iliona wagonjwa 122,362 kati ya hao watu wazima walikuwa 111,542 na watoto 10,820 na kati ya hao wagonjwa waliolazwa walikuwa 4,407 wakiwamo watu wazima 3,286 na watoto 1,121.

“Watoto tuliowafanyia upasuaji walikuwa na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika mpangilio wake na matatizo ya valvu,” alisema Dk Kisenge

Habari Zifananazo

Back to top button