JKCI yaokoa Sh milioni 493 upasuaji mfumo wa umeme wa moyo

JUMLA ya wagonjwa 15 wenye matatizo katika mfumo wa umeme wa moyo wamefanyiwa upasuaji na wengine kuwekewa betri katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na kiasi cha Sh milioni 493 zimeokolewa kutokana na huduma hiyo kutolewa ndani ya nchi.

Gharama ya matibabu kwa wagonjwa 15 ni Sh milioni 253 lakini kama wangepelekwa nje ya nchi kama India au Afrika Kusini ingegharimu Sh milioni 746. Kambi hiyo ya matibabu ilianza Aprili 24 hadi jana ambapo madaktari wa JKCI walishirikiana na madaktari kutoka Marekani.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi mkoani Dar es Salaam, Daktari Bingwa wa Moyo, Yona Gandiye alisema matarajio yao ilikuwa ni kuhudumia wagonjwa 10 lakini kadiri walivyoendelea wamehudumia 15 kutokana na uhitaji mkubwa wa huduma hiyo.

Dk Gandiye alibainisha kuwa kati ya hao, wagonjwa sita wamewekewa betri ya moyo, wawili wamebadilishiwa vifaa vilivyokuwa vimeisha muda, wagonjwa wawili waliwekewa kifaa kinaitwa CRTD kutokana na upande wa kushoto kushindwa kufanya kazi.

Alisema mtambo mpya uliofungwa una uwezo wa kuwasaidia kusoma namna mtiririko wa mapigo ya moyo yanavyotoka ndani ya moyo hasa wale wagonjwa wanaolalamika kuzimia, moyo kwenda haraka sana wakiwa wanafanya kazi na wakabaini tatizo linatoka wapi.

“Tunaishukuru serikali kwa kutupatia mashine hii ya kugundua mwenendo wa mapigo ya moyo na mashine kubwa pia ilinunuliwa na ina uwezo mkubwa, daktari muda wowote anaweza kutoa taswira na umbile la moyo na kugundua hitilafu iko sehemu gani na tunashughulikia sehemu husika,” alifafanua.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge alisema madaktari hao kutoka Marekani wanakuja kufundisha madaktari wenzao na kutibu wagonjwa wenye matatizo ya moyo na wagonjwa 15 wameweza kutibiwa.

Naye Profesa Matthew Sackett kutoka Marekani alisema wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kufanya upasuaji na wagonjwa wanaendelea vizuri na wataendelea kuja na ujuzi mpya kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji upasuaji.

Habari Zifananazo

Back to top button