JKT kubeba kilimo biashara kwa vijana

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema serikali itaunganisha shughuli za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Mpango wa Jenga Kesho iliyobora kwa Vijana (BBT) maarufu kama kilimo biashara kwa vijana.

Rais Samia ameyasema hayo jana wakati akihutubia maelfu ya maofisa, askari, vijana wa JKT na wananchi katika maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa JKT yaliyofanyika Uwanja wa Jamhuri jijini hapa.

Alisema hatua hiyo ni kuwajengea kesho nzuri ya vijana, kuongeza fursa za vijana kujitegemea na kushiriki kikamilifu shughuli za kilimo, ufugaji, uvuvi na uchumi wa buluu.

Advertisement

Rais Samia alisema serikali inakuja na programu nyingi za kuwainua vijana na kuwa kwa sasa inatekeleza Programu ya BBT, na kuwa mpango wa sasa ni kuunganisha shughuli za JKT kuingia kwenye mpango huo ili vijana wawe na mwelekeo mzuri wanapomaliza mafunzo yao.

“Nafarijika kuona kwa sasa mwamko wa vijana kujiunga na mafunzo ya lazima ni mzuri na tutaendelea kuwawezesha ili kuendelea kuchukua vijana wote,” alisema Rais Samia. Aliongeza: “Lengo la serikali ni kuunganisha shughuli zinazofanywa na JKT kuingia kwenye mpango huu.

Tunaposema tunakwenda kukarabati makambi zaidi, mbali na mafunzo ya ukakamavu na ya kijeshi yataungana na mafunzo ya BBT ili kuwajengea kesho nzuri vijana ili wanapotoka pale wajue wanakwenda wapi na wanakwenda kufanya nini, kinyume na sasa vijana wakitoka hawakupata nafasi ya ajira, wanazubaa mitaani.

” Rais Samia ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu, alisema msukumo wa kuanzishwa kwa jeshi hilo Julai 1963, ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na vijana wenye utayari wa kulitumikia taifa lao. “Kutokana na umuhimu wa JKT katika kuwaandaa vijana, mwaka 1964 wakati akiwahutubia vijana wa JKT kwenye Kambi ya Mgulani, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alisisitiza kwamba JKT litakuwa lango kuu kwani kila kijana atalazimika kulipita kabla ya kwenda kulitumikia taifa katika nafasi mbalimbali.

Na huu ndio mwelekeo wetu,” alibainisha Rais Samia. Aliongeza: “Ndio maana mwaka huu idadi ya vijana waliojiunga JKT wameongezeka na kila mwaka idadi itaendelea kuongezeka tofauti na wale wanaokwenda kwa hiari.” Alisema katika kipindi cha miaka 60 ya kuwapo kwa JKT, imekuwa ikitekeleza majukumu yake ya msingi ya kuwajenga vijana kiutayari kulitumikia taifa lao kwa kujenga umoja, uzalendo, nidhamu na uadilifu. Alisema JKT inawafunza vijana kuingia katika maeneo mengine ya kazi kwa kujitegemea ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa.

“Kwa sasa tunatekeleza Dira ya nchi yetu ya mwaka 2020-2025 ambayo imeelekeza kujenga uzalendo, utaifa na umoja, lakini pia JKT inatekeleza Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano unaotekelezwa nchini ambao unatakiwa kumalizika 2026/2027,” alisema.

“Mpango huu umehimiza mambo kadhaa, lakini jambo kubwa ni kuchagiza kutimiza wajibu wetu wa kutumia rasilimali zetu za ndani ili kuondoa utegemezi bila kusahau mila na desturi zetu. Mpango huo umesisitiza kuendeleza kuimarisha vyuo vya ufundi au stadi za maisha shughuli ambazo nyingi zinafanywa na JKT.” Alisema katika Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano unahimiza uwezeshaji vijana uliogawanyika katika maeneo mbalimbali likiwamo la kuwawezesha vijana kufunguka kiuchumi. Alisema JKT imekuwa ikitengeneza ajira jambo ambalo limesisitizwa kwenye mpango huo wa maendeleo kwa lengo la kuwawezesha vijana kupunguza utegemezi ili nchi ijiendeshe.

Aidha, alisema azma ya serikali ni kuongeza uwezo wa JKT iendeshe majukumu yake ya kuwalea vijana vizuri, huku akieleza faraja yake baada ya idadi ya vijana kuomba kujiunga JKT kuendelea kuongezeka. “Sote ni mashahidi kwa kazi kubwa zilizotukuka ambazo JKT imezifanya katika taifa letu ambazo ni ujenzi wa miradi mikubwa, uokozi kwenye maafa na kazi mbalimbali za kujitolea,” alieleza.

Alisema serikali imedhamiria kuiwezesha JKT kuwa ya kisasa zaidi yenye kuendana na mahitaji ya sasa katika kutimiza majukumu ya malezi ya vijana kuwajengea uzalendo wenye kulithamini taifa, kujitegemea uzalishaji mali na kulitetea taifa bila hofu.

Alizitaja baadhi ya kazi hizo zilizofanywa na JKT ni ujenzi wa ukuta kuzunguka migodi ya madini ya tanzanite iliyopo Mirerani mkoani Manyara, Mji wa Serikali, Mtumba na Ikulu ya Chamwino.

Amelipongeza Shirika la Uzalishaji Mali la JKT (SUMA JKT) kwa namna linavyoshiriki shughuli za kibiashara, kutoa gawio na kulipa kodi mbalimbali za serikali; huku akiagiza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kuandaa mpango mkakati wa kurekebisha makambi ya jeshi yanayohitajika

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *