JKT kutoa matibabu ya afya bure
KATIKA kuadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), jeshi hilo linatoa huduma za afya bure na uchangiaji wa damu ambapo zaidi ya chupa 10,000 zinatarajiwa kukusanywa.
Akizungumza wakati wa uchangiaji damu na utoaji wa huduma za afya ambao utafanyika kwa siku mbili katika viwanja vya SumaJKT House jijini hapa, Mkuu wa Huduma za Sheria wa JKT, Kanali Projest Rutaihwa alisema katika maadhimisho hayo jeshi limeamua kutoa huduma kwa jamii na uchangiaji wa damu.
“Kwa hapa Dodoma tunatoa huduma za afya bure kwa kushirikiana na wadau wengine lakini pia tunachangia damu ambapo maafisa, askari na vijana wa JKT kwa mujibu wa sheria na raia tushiriki kutoa damu.”
“Hii inaonesha tayari vijana wetu wameiva kwa uzalendo wa kujitolewa damu ili kuokoa maisha ya watu wengine,” alisema na kuongeza kuwa utaratibu wa kuchangia damu unafanyika katika makambi yote ya JKT nchini.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka JKT, Meja Yusuf Sasamalo alisema kwa Dodoma uchangiaji wa damu unafanywa na maafisa, askari na vijana wa kwamujibu wa sheria kutoka kikos 834 JKT Makutupora na raia ambapo chupa 500 zinatarajia kukusanywa.
“Kwa hapa Dodoma tunatarajia kukusanya chupa 500 lakini kwa vile kazi ya uchangiaji wa damu unafanywa pia kwenye makambi mengine ya JKT badi makadirio ni kukusanya zaidi ya chupa 10,000,” alisema.
Naye Mkuu wa Kitendo cha Damu Salama kutoka Hospital ya Benjamin Mkapa, Kucy Kibaja alishukuru JKT kwa kushiriki katika uchangiaji damu na kuwa wamekuwa wakifanya hivyo kila wakati kutokana na wao kutambua umuhimu wa kuchangia damu kwa wananchi.
“Hivyo niwashukuru sana Jeshi la Kujenga Taifa kwa kuwa mstari wa mbele katika kuchangia damu, nitoe rai kwa taasisi zingine kufanya hivyo hasa tukitambua kuwa hakuna kisima cha kuchimba damu zaidi ya mimi na wewe.
”