JKT na mkakati kupunguza Uhaba wa mafuta ya kula

KIGOMA: MKUU wa Tawi la Utawala wa jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema Jeshi hilo linaendelea na mpango mkakati wake kulima mazao ya kimkakati likiwemo zao la mchikichi ili kuisaidia Serikali kupunguza gharama za kuagiza mafuta nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya uzalishaji wa zao hilo katika Kikosi cha Jeshi 821 Bulombora kilichopo mkoani Kigoma, Brigedia Jenerali Mabena amesema,kutokana na uzalishaji wa zao la mchikichi unaofanywa na kikosi hicho,utaenda kupunguza gharama hizo mara baada ya kuanza mavuno.

Brigedia Jenerali Mabena ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi amesema JKT imeandaa shamba la ukubwa wa ekari 2000 huku akisema tayari ekari 1100 zimeshapandwa na kwamba wanaendelea kuhakikisha ekari 900 zilizobaki nazo zinapandwa.

Vile vile amesema JKT kwa kushirikiana na TARI Kigoma waliandaa vitalu vya mbegu ambapo miche zaidi ya 300,000 imeshagawiwa kwa wananchi lakini pia umoja wa wakulima AMCOS Kigoma nao wamenufaika na mbegu ambazo walipata bure.

Brigedia Jenerali Mabena ametumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ambao wamekuwa wakiyasimamia maagizo hayo katika kuhakikisha mazao ya kimkakati hasa ya  mazao ya mafuta yanakwenda vizuri.

Akizungumzia kuhusu kilimo cha mazao ya chakula amesema kwa upande wa mahindi wamefanikiwa katika lengo la kulisha vijana na hivyo kupunguza bajeti ya Serikali katia eneo hilo.

Kwa upande wa mpunga (mchele) amesema wamefika asilimia 50 huku akisema bado wanaendelea kuongeza mashamba yao hasa kikosi 837 Chita JKT.

Ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaongezea nguvu ili kuleta tija katika kilimo cha zao la mpunga.

Kuhusu zao  la maharagwe amesema kutokana na mabadiliko ya tabianchi hawakuweza kufikia lengo lakini hata hivyo mpango wao ni kuendelea kuongeza uzalishaji.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button