JKT: Tumefanikiwa, tunaaminika

MKUU wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele amebainisha mafanikio lukuki ya jeshi hilo ndani ya miaka 60 likiwamo la kuaminiwa.

Akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa JKT Julai 10, 1963 yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma jana, Meja Jenerali Mabele alisema jukumu la msingi la jeshi hilo ni malezi ya vijana, uzalishaji mali na ulinzi wa taifa, na kuwa tangu kuanzishwa kwake linatekeleza majukumu kwa ufanisi.

Meja Jenerali Mabele alisema kwa sasa mafunzo ya vijana yanaendelea kwa operesheni mbili za vijana wa mujibu wa sheria za Operesheni Samia na Venance Mabeyo, na Operesheni Miaka 60 ya JKT kwa vijana wa kujitolea.

Advertisement

Alisema JKT imefanikiwa kubadili fikra za kikoloni kwa vijana waliohudhuria mafunzo, kujenga umoja, moyo wa kupenda kazi, uadilifu, nidhamu na kudumisha uhuru na amani ya Taifa.

Alisema pia JKT imeongeza idadi ya vijana wanaojiunga kupata mafunzo ya lazima kutoka vijana 11 mwaka 1963 mpaka 52,000 ambao wako kambini kwa sasa.

Meja Jenerali Mabele alisema kutokana na kuaminiwa, JKT imetekeleza miradi ya kimkakati ukiwamo ujenzi wa Ikulu ya Chamwino na majengo ya serikali.

Alisema katika kuhakikisha jeshi hilo linajilisha kwa chakula na kuchangia usalama wa chakula nchini, JKT inatekeleza mradi wa skimu ya umwagiliaji ambayo iko katika hatua za mwisho za ukamilishaji. Meja Jenerali Mabele alisema JKT imejihusisha kuzalisha mali kupitia vikosi na Shirika la Uzalishaji Mali (Suma JKT) katika sekta za ujenzi, kilimo, ufugaji, uvuvi na biashara hivyo kuchangia gharama za mafunzo ya vijana, kutoa gawio serikalini, kulipa kodi na kuongeza ajira.

Pia alisema jeshi hilo linakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwamo ufinyu na uchakavu wa miundombinu kwenye kambi zake, upungufu wa wataalamu, uhaba wa vifaa na mtaji mdogo kwa Suma JKT. Meja Jenerali Mabele aliishukuru serikali kwa kuliwezesha jeshi hilo uwezo wa kibajeti kila mwaka.

JKT imemtunuku tuzo Rais Samia Suluhu Hassan na waasisi wa taifa; Julius Nyerere ambaye ni Rais wa Kwanza wa Tanzania na Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

1 comments

Comments are closed.

/* */