JKT yajiimarisha sekta ya ujenzi

MKUU wa Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) Meja Jenerali, Rajabu Mabele amezindua rasmi mitambo mikubwa ya kuzalisha na kusafirisha zege itakayokuwa ikitumiwa na kampuni ya ujenzi ya Shirika la Uzalishaji Mali (SUMAJKT).

Mitambo hiyo ambayo itaimarisha sekta ya ujenzi katika Shirika hilo imegharimu zaidi ya Sh bilioni 1.349.

Akizungumza mara baada ya kuzindua mitambo hiyo Meja Jenerali Mabele amewaagiza watendaji wa SUMA JKT kuhakikisha wanasimamia mitambo hiyo ili ilete tija iliyokusudiwa katika kuongeza ufanisi wa SUMAJKT katika sekta ya ujenzi.

Advertisement

“Kwa watakao pewa dhamana ya kusimamia mitambo hiyo lazima wazingatie matengenezo kwa wakati ili mitambo hiyo idumu kwa muda mrefu sio ukiona mtambo unafanya kazi unaendelea kuutumia hali ukijua muda wa matengenezo umefika.”

Amesema kuwa JKT inakwenda kuadhimisha miaka 60 tangu kuasisiwa kwake na sasa ni wakati wa kuwa na teknolojia za kisasa.

“Ni lazima tuoneshe mabadiliko kwa kuwa na vifaa vya kisasa katika kutekeleza majukumu na hasa ikizingatia kuwa SUMA JKT ilianza kama kitengo cha ukarabati lakini kilikuwa na sasa ni shirika kubwa sana hapa nchini na linaloaminika na linalopata miradi mikubwa hivyo lazima tuonyeshe utofauti.”

“Mwanzo tulikuwa tunaingiza vijana wengi mashambani lakini kwa sasa tumeweka mitambo mikubwa ya kiteknolojia ya kisasa mashambani na tunalima kwa tija kubwa kutokana na mitambo tuliyonayo.”

Amesema awali shirika lilikuwa likiingia gharama kubwa katika kununua zege na kokoto na kwa kutumia mitambo hiyo SumaJKT itaondoa changamoto hiyo na tutakuwa tunajutegemea. Mwelekeo wetu ni kuendelea kununua mitambo mingine na krasha ya kutengeneza kokoto ili kuendelea kupunguza gharama za uendeshaji wa shirika.

Ameongeza kuwa “tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kuiamini SUMAJKT kwa kuipa miradi mingi na ndio maana wamejipanga kuhakikisha wanapata mitambo ili kutekeleza miradi hiyo kwa ufanisi na kuendelea kuilinda imani hiyo.”

Awali msimamizi wa miradi ya ujenzi wa SUMAJKT, Mogan nyoni amesema mitambo hiyo imeingizwa nchini Januari 16, 2023 na kumaliza kusimikwa Mei 22, 2023 jijini Dodoma.
Alisema mitambo hiyo inauwezo wa kuzalisha zege mita za ujazo 60 kwa saa, magari matatu yenye uwezo wa kubeba zege mita za ujazo 8 kila moja na pampu ya kusukuma zege.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa SUMAJKT, Kanali Petro Ngata amesema mitambo hiyo itasaidia katika kutekeleza miradi wanayopata na wamejiwekea malengo ya kuongeza vitendea kazi kwa kampuni tanzu za SUMAJKT kuziwezesha kampuni hizo ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.

Ameongeza kuwa “ awali tulikuwa tukinunua zege katika kutekeleza miradi yetu lakini sasa tutatumia mitambo yetu kuzalisha zege na tutaweza kuhudumia makampuni mengine ya ujenzi katika jiji la Dodoma.”

Naye Mwenyekiti wa bodi ya washauri wa SUMAJKT Meja Jenerali Mstaafu Farah Mohamed ameipongeza Shirika kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kutekeleza yote wanayokubaliana katika vikao vya bodi na Shirika hilo.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *