Jokate azindua kiwanda cha nafaka Mtwara

MTWARA: KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Jokate Mwegelo (MNEC) amezindua kiwanda cha kuchakata nafaka cha Anno Domini Food Industries kilichopo Manispaa ya Mtwara mikindani mkoani Mtwara.

Hayo yamekuja wakati Katibu Mkuu huyo alipokuwa katika ziara ya kikazi mkoani humo na kupokelewa na wananchi kutoka mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma na kupata fursa ya kutembelea baadhi ya miradi mbalimbali ya maendeleo katika manispaa hiyo.

Mkurugezi wa Kiwanda hicho Thobias Aloyce amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kujiajiri.

Amesema kiwanda hicho kinaenda Kufungua fursa kwa vijana wengi kwani mpaka sasa kimeajiri vijana 10 na kikianza kazi rasmi kinatarajia kuajiri zaidi ya vijana 20 huku akiitaja moja ya changamoto inayowakabili ikiwemo masoko.

“Malengo yetu, tunatarajia kufungua kiwanda kingine zaidi ya hiki kama mambo yakienda vizuri Mungu akijaalia na pia tunatarajia kufungua kiwanda kingine cha kukamua mafuta ya karanga, alizeti lakini changamoto yetu kubwa ni masoko,” amesema Thobias.

Akizungumza kwa niaba ya Jumuiya hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Abdi Mahmoud Abdi amepongeza uwekezaji wa kiwanda hicho kwani ni fursa kwa wananchi wa mkoani humo hususani vijana huku akiahidi kwamba changamoto zote zinazowakabili kiwandani hapo zitawasilishwa kwenye mamlaka husika ili ziweze kufanyiwa kazi.

“Lakini pia naomba niwaahidi vijana katika kiwanda hiki, Changamoto zote zilizowasilishwa tutaziwasilisha kwenye mamlaka husuka kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi na tumefurahi sana sana uthubutu wa vijana wenzetu uliyofanywa katika kiwanda hiki…Sisi vijana akili zetu tunayo maarifa mengi sana yanayotupelekea kutatua changamoto zetu ila tatizo moja tu, tunaogopa kuthubutu “amesema Mahmoud

Hata hivyo, Mwegelo amewaahidi vijana hao kuwa UVCCM chini ya Mwenyekiti wake, Mohammed Ali Kawaida (MCC) milango yake ipo wazi wakati wote kuwasemea vijana wa kitanzania hivyo wasisite kubisha hodi pale wanapoona kuna changamoto ya aina yoyote inayohitaji utatuzi.

Habari Zifananazo

Back to top button