TANGA,Korogwe: Katibu Mkuu wa Jumuiya ya wanawake wa Chama cha Mapinduzi UWT Taifa, Jokate Mwegelo amewaaga Wananchi wa Wilaya ya Korogwe alipokabidhi ofisi kwa Mkuu wa Wilaya mpya.
Katika tukio la kuwaaga Wananchi wa Korogwe, Jokate amekabidhi mitungi mikubwa ya gesi ya Oryx 140 pamoja na majiko yake bure kwa wanawake wajasiriamali 574 waliopo wilayani hapo.
Akizungumza leo jijini Tanga wakati akikabidhi mitungi hiyo iliyotolewa na Kampuni ya Oryx Gas kwa kushirikiana na kampuni ya Coca- cola Jokate amesema mitungi hiyo itumike katika kuboresha biashara na chachu ya kuleta maendeleo kwenye matumizi ya nishati safi.
“Ni imani yangu msaada huu utakuwa ni chachu ya kuweza kuongeza bidii katika utafutaji lakini niwaombe uwekezaji huu uwe endelevu na chachu ya ukombozi wa matumizi ya nishati mbadala kwa mama lishe”amesema Katibu Mkuu huyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Korogwe William Mwakilema amesema kuwa serikali inatambua mchango wa mamalishe katika harakati za ukuwaji wa uchumi wa nchi hii.
Hata hivyo Mkurungenzi wa mahusiano kutoka coca-cola kwanza Salum Nassor amesema kuwa msaada huo ni katika kuunga mkono dhamira ya serikali kuwa ifikapo mwaka 2030 matumizi ya nishati safi kufikia angalau 80% nchini nzima.