Juhudi za amani Sudan zaanza Saudi Arabia

OFISA Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya kibinadamu Martin Griffiths, aliwasili katika Jiji la Jeddah, Saudi Arabia siku ya Jumapili kwa mazungumzo yanayolenga kusitisha mapigano kati ya makundi ya kijeshi yanayopigana nchini Sudan;

Griffiths yuko Jeddah “kujihusisha na masuala ya kibinadamu kuhusiana na Sudan,” msemaji wa Umoja wa Mataifa Eri Kaneko alisema.

Wawakilishi kutoka majeshi yanayopigana nchini Sudan wamewasili Saudi Arabia kwa mazungumzo yao ya kwanza ya ana kwa ana.

“Mazungumzo ya awali” kati ya jeshi la Sudan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) yalikuwa yaanze Jumamosi huko Jeddah.

Mazungumzo hayo yanafadhiliwa na nchi ya Marekani na Saudi Arabia.

Pande zote mbili zimesema zitajadili usitishaji wa amani wa kibinadamu, lakini sio mwisho wa mzozo huo.

Mikakati kadhaa ya kusitisha mapigano imesambaratika tangu mapigano hayo yaanze wiki kadhaa zilizopita.

Hakujakuwa na neno hadi sasa kuhusu iwapo mkutano huo umefanyika au wawakilishi wa pande zote mbili ni akina nani.

Mazungumzo ya Jumamosi yanakuja huku kukiwa na ripoti za kuendelea kwa mapigano katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum. 

Mamia ya watu wameuawa na takriban raia 450,000 wameyahama makazi yao tangu mapigano hayo yaanze.

Habari Zifananazo

Back to top button