WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene amesema juhudi za kukabiliana na ukatili dhidi ya watoto katika zama za utandawazi zinahitaji msukumo mpya na wa pamoja.
Waziri Simbachawene ameyasema hayo wakati akiongoza Mkutano wa kupitia tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto 2017/18- 2021/22 (MTAKUWWA), uliofanyika Ukumbi wa mikutano wa St. Gaspar jijini Dodoma Januari 26, 2023.
Amebainisha kuwa athari za utandawazi zimedhoofisha mifumo ya ulinzi na usalama wa watoto, hivyo kufanya kundi hilo kutokuwa salama, kwani tatizo la ukatili bado ni changamoto katika ngazi zote.
” Kutokana na changamoto hiyo, Wadau wote tuna wajibu wa kuchukua hatua za kudhibiti na kukabiliana na wimbi la vitendo vya ukatili dhidi ya watoto katika maeneo yote, ikiwemo shuleni na nje ya shule. Changamoto yoyote inayoathiri ukuaji wa wa watoto, inachangia kuandaa nguvu kazi dhaifu isiyokuwa na tija kwa jamiii,” amesema Simbachawene.
Waziri Simbachawene ametoa wito kwa wadau kuwa wavumilivu na kuwahakikishia kuwa, katika mkutano wa mawaziri ujao ambao utapitisha rasimu ya MTAKUWWA II, utazingatia sana maoni ya wadau.
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima, amebainisha kuwa taarifa ya tathmini ya MTAKUWWA imekamilika na imeainisha maeneo muhimu yanayopendekezwa kutekelezwa kwa mpango ujao, hivyo kikao hicho kinalenga kuipitia na kuboresha ili kuongeza ufanisi.
“Nawaomba Wadau wote kuwa na subira wakati majadiliano ya tathmini yakiendelea, kwani wote tunajenga nyumba moja,” amesisitiza Waziri Gwajima.