Jukata wamuangukia Rais Samia

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga

JUKWAA la Katiba na Sheria Tanzania (JUKATA), limeomba kuonana na Rais Samia Suluhu Hassan ili kuzungumzia Demokrasia nchini na R4 anazozisimamia Rais.

Wakizungumza kwenye ukumbi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) leo Agosti 15,2023 wadau wa haki za binadamu wamesema Rais Samia ana nia njema za kuboresha demokrasia nchini lakini anarudishwa nyuma na watendaji wachache.

Mwenyekiti wa Jukata, Ananilea Nkya akizungumza amesema Rais Samia kwa moyo wa dhati kabisa alitangaza kusimamia R4 ambazo ni ‘reconciliation, resilience, reforms rebuilding’ yaani ameamua kujenga nchi yenye watanzania wanaoishi kwa kusameheana, kuvumiliana, kuleta mabadiliko na kujenga nchi kwa pamoja

Advertisement

“Lakini kuna wasaidizi wake wachache wanampotosha Rais, wanatweza utu wa Rais, wanadhani kwa kutoa matamko yasiyo na tija na yanayoleta taharuki katika Taifa   letu wanamfurahisha Rais, lakini ukweli ni kuwa wanamtengenezea Rais Samia chuki kwa wananchi, wanamtengezea vinyongo, wanatakiwa kumsaidia Rais na sio kuwa machawa.”Amesema

Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Anna Henga akisoma taarifa ya pamoja ya wadau hao wa haki za binadamu wameliomba jeshi la Polisi kuwaachia watu wote wanaodaiwa kukamatwa na jeshi hilo kutokana na ukosoaji wao katika mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai (IGA).

Amedai waliokamatwa ni Dk Willbroad Slaa, Peter Madeleke, Boniphace Mwabukusi na Mdude Nyagali.

Wadau hao walioungana kwa pamoja ni Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC) pamoja na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS).

Henga ametoa wito wa kumuomba Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuingilia kati suala hilo  ili watuhumiwa waachiwe bila masharti.

Pia wamelitaka Jeshi la Polisi kuheshimu haki na uhuru wa kutoa maoni huku wakisisitiza mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande kuhusu mfumo wa haki jinai nchini yaheshimiwe.

7 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *