Jukwaa la Wakulima Afrika laipa 5 Tanzania

JUKWAA la Kikanda la Wakulima, Kusini mwa Afrika limempongeza serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa ongezeko kubwa la bajeti ya sekta ya kilimo na mpango wa kukuza kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

Wakizungumza jijini Dar es Salaam leo Novemba 24, 2022 katika Mkutano wa Jukwaa hilo, Rais wa Jukwaa hilo Elizabeth Nsimadala na Mwenyekiti Dkt Sinare Sinare kwa nyakati tofauti wamempongeza Rais Samia kwa ongezeko la bajeti ya kilimo kwa zaidi ya asilimia 300.

Advertisement

Ili kufikia ajenda 10/30, Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi bilioni 954 mwaka 2022/2023, ambalo ni ongezeko la zaidi ya asilimia 300

“Fedha alizotenga Rais Samia, zimejumuisha uzalishaji wa haji wa mbegu bora, ruzuku ya mbolea,utafiti wa kilimo na programu ya kilimo kwa vijana, nchi nyingine za Ukanda huu wa Kusini mwa Afrika ziige mfano huu wa serikali ya Tanzania katika katika kusimamia kwa dhati ukuaji na maendeleo ya sekta ya kilimo.”Amesema

Lengo kuu la Jukwaa hilo la Kikanda la Wakulima  ni  kuwakutanisha wakulima kupitia vikundi vyao, kujadili fursa na changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao ya kusaidia wakulima wadogo kuboresha maisha yao, kuimarisha usalama wa chakula na lishe na kupunguza umaskini vijijini.

Nae, Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde akifungua mmkutano huo amesema  mfumo wa kuwaunganisha wakulima wadogo kuunda ushirika ni nyenzo sahihi itakayosaidia wakulima wadogo kunufaika na mazao yao wanayozalisha kutokana na uhakika wa upatikanaji wa masoko, upatikanaji wa mikopo na pembejeo za kilimo kwa wakati.

“Sisi kama Serikali, kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025 tumeainisha mkakati wa kuimarisha ushirika ili uweze kuwasaidia wakulima wadogo katika ukusanyaji wa mazao na utafutaji wa masoko ya uhakika.

“Ni imani yetu kuwa, ushirika utaenda kuongeza kipato cha wakulima wadogo ambao wengi wao wanaishi vijijini na kuwakwamua kwenye lindi la umaskini.

Amesema serikali kupitia Wizara ya Kilimo, inatekeleza Ajenda 10/30 ambayo inalenga kuongeza ukuaji wa kilimo kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

“Kupitia ajenda 10/30, tumejipanga kutekeleza vipaumbele mbalimbali vikiwemo utafiti, kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za kilimo, kuimarisha huduma za ugani, kujenga miundombinu ya umwagiliaji, ujenzi wa maghala ya kuhifadhi mazao, kuongeza mapato ya nje ya kilimo kutoka Dola ya Kimarekani bilioni 2 mpaka bilioni 5, upatikanaji wa masoko ya uhakika na kuongeza upatikanaji wa mitaji kwenye sekta ya kilimo.

Katika  kuhakikisha Ajenda 10/30 inafikiwa, Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi bilioni 954 mwaka 2022/2023, ambalo ni ongezeko la zaidi ya asilimia 300. Fedha hizo, kiasi kubwa zimeelekezwa kwenye ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji”Alisema Mavunde

Naye Makamu wa Rais wa Shirika la IFAD anayeshughulikia Mahusiano ya Nje na Utawala, Mhe. Satu Santala alieleza kuridhishwa na namna Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyoshirikiana na sekta binafsi na hususani jitihada za kuimarisha ushirika nchini ili uweze kuwa na manufaa makubwa kwa wananchi, ambao wengi wao ni wakulima na wanaishi vijijini.

Pia  ametaka mkutano huo utoke na maazimio ambayo yatasaidia kutatua matatizo ya msingi ya sekta ya kilimo katika Bara la Afrika hasa changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi, uhakika wa usalama wa chakula,upotevu wa mazao baada ya mavuno na matumizi hafifu ya teknolojia mbalimbali za kilimo.