Jumuiya ya wazazi Geita yapatiwa baiskeli 50

JUMUIYA ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Geita imepatiwa usafiri wa baiskeli 50 kwa ajili ya kuwasaidia makatibu wa jumuiya ya wazazi kata kuwafikia wanachama.

Baiskeli hizo zimetolewa na kukabidhiwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) Wilaya ya Geita, Chacha Wambura mbele ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa.

Chacha amesema baiskeli hizo ni ombi la wajumbe wa jumuiya hiyo wilayani humo walilotoa hivi karibuni katika kikao cha Baraza la Jumuiya ya Wazazi kulenga kuondoa changamoto ya usafiri.

Amesema baiskeli zitagawiwa kwa makatibu wa jumuiya kwenye kata zote 50 za Wilaya ya Geita kwa ajili ya kusikiliza kero za wanachama na kusaka wanachama wapya wa CCM.

Amesema pia ametoa msaada wa matengenezo ya pikipiki mbili, mali za jumuiya hiyo kuwasaidia viongozi wakuu wa Jumuiya ya Wazazi wilaya kufanya kazi na kuwafikia wananchi kwa wakati.

Chacha ameongeza, jumuiya hiyo ameipatia kompyuta zitakazotumika kwa shughuli za kiofisi yote hayo ikiwa ni mikakati ya kuimarisha utendaji wa jumuiya kabla na baada ya uchaguzi.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Nicolous Kasendamila amempongeza Chacha kwa kujitolea usafiri huo na kuwaomba wanachama, viongozi na wadau wengine kujitolea.

Kasendamila amekemea mitazamo hasi kwa watu wanaotoa misaada CCM kwamba wanataka nafasi kugombea ubunge na kueleza chama kina misingi na taratibu zake za kupata wagombea.

“Wachangiaji wote tunawakaribisha waendelee kujitolea kwa ajili ya kukijenga na kukiimarisha chama chetu, masuala ya kugombea sisi tunaheshimu taratibu na katiba.”

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Geita, Robert Nyamaigolo amesema baisikeli hizo zitagawiwa kwenye majimbo matatu, ambayo ni Geita mjini, Geita vijijini na Busanda.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Fadhil Maganya amesema msaada wa usafiri wa baiskeli ni jambo lenye tija katika kuendelea kukijenga chama kuelekea uchaguzi mpya.

Ameelekeza kwamba baiskeli hizo ni mali ya chama na kila mwanachama wa CCM anayo nafasi ya kutumia kwa maslahi ya CCM na asitokee mtu akajimilikisha baiskeli hizo.

Habari Zifananazo

Back to top button