Jwaneng watua kumvaa mnyama

DAR ES SALAAM: KLABU ya Jwaneng Galaxy ya nchini Botswana imetua nchini salama kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam kwaajili ya kukabiliana na Simba SC katika mchezo wa mwisho hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) jumamosi hii.

Kuwasili kwa Jwaneng siku nne kabla ya kipute hicho kilichobatizwa jina la ‘vita ya kisasi’ katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, inaipasa Simba kushinda mchezo huo ili kufuzu hatua ya robo fainali ya CAFCL kwani watakuwa na jumla ya alama 9 kibindoni.

Iwapo, Jwaneng Galaxy wakishinda, watajikusanyia alama 7 huku wakiiombea Wydad Casablanca ipoteze dhidi ya ASEC Mimosas ili kusonga mbele.

Advertisement

Ni mechi ya mwisho ya wawili hao katika kampeni ya hatua ya makundi huku ASEC Mimosas wakiwa ndio timu pekee katika Kundi B kutinga hatua robo fainali baada ya kuvuna alama 11 katika michezo mitano.

Timu tatu zilizosalia kila moja zina nafasi ya kufanikiwa ikiwa zitapata alama za juu zaidi katika mechi zijazo.

Endapo Simba itashinda itafikisha alama 9 katika michezo sita huku ikisubiri kujua matokeo kati ya Wydad Casablanca dhidi ya ASEC Mimosas.

Iwapo Wydad Casablanca watafanikiwa kushinda katika uwanja wake wa nyumbani, watakuwa na alama 9 sawa na Simba. Matokeo ambayo yatawabeba wawakilishi wa Tanzania kwa kuwa waliopata matokeo bora zaidi walipokutana.

Katika mechi yao ya kwanza katika Uwanja wa Marrakesh huko Morocco, Simba ililala kwa bao 1-0 huku katika mchezo wa marudiano uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini hapa, mnyama aliibuka na ushindi wa mabao 2-0.