JWT: Lipeni kodi kwa wakati

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Taifa (JWT), Hamis Livembe amewataka wafanyabishara nchini kulipa kodi kwa hiari kwa maslahi mapana ya taifa.
Aidha, amewashauri kufanya kazi kwa bidii kwa sababu Rais Samia Suluhu Hassan ameifuangua nchi kiuchumi na kutoa fursa ya kusikiliza kero zao.
Livembe ameyasema hayo leo Novemba 7, 2023 wilayani Kisarawe mkoani Pwani, wakati wa mkutano wake na wafanyabiashara wilayani humo wa kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu ili kufanyabiashara kwa utulivu bila kuwapo kwa migomo ya mara kwa mara.
“Tupo Mkoa wa Pwani kwa ajili ya ziara zetu za kawaida za kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari lakini pia kutumia vizuri fursa tuliyopewa na serikali inayoongozwa na mama yetu, Rais Samia kusikiliza changamoto za wafanyabiashara na kukaa mezani kuzitatua.
“Mama hataki ugomvi anataka apate chake cha halali na sisi tulipe cha halali, ametushushia faini ya makosa ya kutokutoa risiti za EFD kutoka Sh. milioni 4.5 hadi Sh. milioni 1.5 .” amesema Livembe.
Amesema ni jambo la kheri na la kupongezwa kwa kupunguzo hilo kubwa la zaidi ya asilimia 60 na kilikuwa kilio kikubwa cha wafanyabishara nchini.
Aidha, amesema jambo lingine kubwa lillilofanyiwa kazi na serikali ni kupungua kwa kodi ya ongezeko la thamani kutoka mtaji wa Sh. milioni 100 na kupanda kuwa Sh. milioni 200 na lengo likiwa ni kufikia Sh. milioni 500.
Awali wafanyabishara hao walipata fursa ya kueleza kero zao zinazohusu kodi na mazingira ya kufanyia biashara.
Mfanyabishara Christina Mulu, alisema TRA wanatakiwa kuwapa elimu ya kutosha kuhusu ulipaji kodi badala ya kukazania kukusanya bila kuwasikiliza wafanyabishara kwanza.
“Wafanyabiashara wengi hatuna elimu ya kodi, matumizi ya EFD hatujui wakati mwingine risiti zinagoma kutoka na mashine kusumbua sasa TRA wakija wao ni kutaka tu kutoza faini badala ya kutupa elimu kwanza,” amesema Mulu.